• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Mwenyekiti wa Embakasi Ranching azikwa katika shamba lake la Ndeiya

Mwenyekiti wa Embakasi Ranching azikwa katika shamba lake la Ndeiya

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa kampuni ya kununua na kuuza mashamba ya Embakasi Ranching tangu 2019 hadi mwaka huu 2023, Bw James Njoroge anazikwa leo Jumanne kwenye shamba lake la Ndeiya katika Kaunti ya Kiambu.

Mnamo Agosti 30, 2023, Taifa Leo ilichapisha habari kuu ikiangazia namna Embakasi Ranching, imegeuka kuwa uwanja wa mauti tangu ilipoanzishwa 1976 baada ya wenyeviti wake wote kufariki kwa njia ya kutatanisha.

Kampuni hiyo, iliyoanzishwa na rais wa kwanza wa taifa Mzee Jomo Kenyatta, imeongozwa na wenyeviti wanne.

Wenyeviti hao walikuwa; Mbunge wa zamani wa Embakasi, Bw Muhuri Muchiri aliyehudumu kuanzia 1976 hadi 2006, Bw Kariuki Mwaganu (2006-2009), Bw Mwangi Thuita (2010 to 2018) na Bw James Njoroge aliyehudumu 2019 hadi mwaka huu 2023.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa kampuni ya kununua na kuuza mashamba ya Embakasi Ranching tangu 2019 hadi mwaka huu 2023, marehemu James Njoroge anazikwa leo Jumanne, Septemba 5, 2023, kwenye shamba lake la Ndeiya katika Kaunti ya Kiambu. PICHA | MWANGI MUIRURI

Lakini ajabu ni kwamba, wenyeviti hao wote walikufa ghafla na ripoti ya upasuaji wa miili yao ilionyesha kuwa, walikata roho kutokana na mshtuko wa moyo.

Inaonekana kuwa hiyo ndio ilikuwa hatima ya wale walioteuliwa kuongoza ranchi hiyo inayosemekana kumiliki ardhi ya thamani ya mabilioni ya fedha.

“Wadhifa wa mwenyekiti huambatana na changamoto nyingi na ni kana kwamba huwa ni cheo cha mkosi. Mwenyekiti huchaguliwa na wenye hisa kulinda mali yao, ambayo humezewa mate na watu fulani wenye ushawishi serikalini. Hii ndio maana wao hujipata katika njia panda, kupambana na wezi hao huku nao wakipania kufaidika,” akasema Bw Joseph Njenga, mwanachama mmoja wa bodi ya ranchi hiyo.

Vuta nikuvute kati ya wanyakuzi ardhi na wenye hisa wa kampuni hii vimewahi kufikia marais Daniel Moi, Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na sasa William Ruto. Isitoshe, baadhi ya wenyeviti wa kampuni hiyo pia wamewahi kukwaruzana na marais walioko mamlakani.

Kwa mfano, mnamo 2018, Bw Thuita Mwangi alitofautiana na Bw Kenyatta. Hii ni baada ya mwenyekiti huyo, kukaidi amri ya rais huyo (sasa mstaafu) kwamba kampuni hiyo ivunjiliwe mbali na wenye hisa wapewe hatimiliki za ardhi.

Wawili hao walilumbana hadharani mara kadha, rais huyo akishikilia msimamo wake na hata kuzindua mpango wa utoaji hatimiliki, lakini Thuita alikataa akishikilia kuwa hiyo ni kampuni ya kibinafsi.

Mnamo Agosti 2028, Bw Thuita alizirai na kufa katika chumba kimoja cha malazi katika mtaa wa Ruai.

Kabla ya hapo mnamo 1978, Bw Muhuri Muchiri alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa ranchi hiyo alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani na Jaji Fidhussein Abdulla.

Hii ni baada ya kupatikana na hatia ya kuiba kahawa iliyokuwa ikisafirishwa kutoka Malaba hadi Mombasa.

“Kwa kuwa mwandani wa Rais Jomo Kenyatta, ambaye kwa pamoja walianzisha ranchi hiyo, Bw Muchiri hakuamini kwamba angetupwa gerezani,” akasema aliyekuwa mkuu wa mkoa Joseph Kaguthi.

Hata hivyo, baadaye aliachiliwa huru kwa msamaha wa rais.

Bw Kaguthi alisema siasa ziliendelea kuingizwa katika usimamizi wa ranchi hiyo huku baadhi ya watu wenye ushawishi wa kisiasa wakitaka kunyakua sehemu ya ardhi ya kampuni hiyo.

Joto lilizidi huku Bw Muchiri akihangaishwa na magenge ya wanyakuzi, kiasi kwamba alilazimika kukwepa kuishi katika boma lake la kifahari karibu na mji wa Kiambu na badala yake akaamua kulala katika mikahawa mbalimbali jijini Nairobi.

Mnamo Mei 2006 maiti yake ilipatikana katika kimojawapo cha vyumba vya malazi katika baa yake kwa jina Studio 45.

Baada ya kifo cha Muchiri, Bw Thuita alishika hatua ya uongozi wa kampuni hiyo akikumbuna na joto ambalo lilimpata mtangulizi wake.

Yeye pia aliishi maisha ya kukwepa maadui halisi na wengine wa kufikirika waliokuwa wakimezea mate ardhi ya kampuni ya Embakasi Ranching Co Ltd.

Bw Thuita naye alianza kuishi katika mikahawa mbalimbali ambako alipatikana amekufa 2018. Mnamo Aprili 13, 2019 wenyehisa wa kampuni hiyo walimchagua Bw James Njoroge mwenyekiti mpya. Msaibu ya watangulizi wake yaliendelea kumwandama.

Tofauti na hao wengine, waliokufa katika vyumba vya malazi vya kukodisha, Bw Njoroge alifariki akiwa nyumbani kwake kijijini Kabuku, Kaunti ya Kiambu mnamo Agosti 26, 2023.

Kabla ya kifo chake, Bw Njoroge alikuwa ametofautiana na Rais Ruto kuhusiana na kile alichokitaja kama “kitendo haramu cha kupeana hatimiliki za ardhi kwa ardhi ya kampuni ya ranchi ya Embakasi”.

  • Tags

You can share this post!

Tabianchi: Rais Ruto asema wakati wa vitendo ni sasa

Polisi wafungiwa ndani ya nyumba ya mshukiwa wa kuuza...

T L