• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
NEMA yataka maoni yatolewe kuhusu ujenzi wa hoteli ya Raila

NEMA yataka maoni yatolewe kuhusu ujenzi wa hoteli ya Raila

NA VALENTINE OBARA

MAMLAKA ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA), imetoa wito kwa umma kuwasilisha maoni kuhusu mpango wa kampuni ya kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, kujenga hoteli Malindi.

Kampuni ya Kango Enterprises Ltd, ambayo Bw Odinga ni mmoja wa wakurugenzi, imenuia kujenga hoteli hiyo kando ya bahari katika eneo la Mayungu, Kaunti ya Kilifi.

Kwenye notisi iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali, Mkurugenzi Mkuu wa NEMA, Bw Mamo Boru Mamo, alithibitisha kupokea ripoti ya kutathmini athari za mazingira kuhusu mradi huo.

Wananchi walipewa siku 30 kuwasilisha maoni yao kwa NEMA kuhusu ujenzi huo, kwa mujibu wa notisi hiyo iliyochapishwa Ijumaa iliyopita.

Baadhi ya athari za kimazingira ambazo zinatarajiwa kutokana na mradi huo ni ukataji wa miti, uharibifu wa mazingira halisi na utupaji taka.

Hata hivyo, mpango wa ujenzi umejumuisha mapendekezo ya kuepusha uharibifu wa mazingira ikiwemo kwa kupanda miti katika sehemu ambazo hazitakuwa na majengo, kushirikisha msimamizi wa taka aliyeidhinishwa na NEMA, miongoni mwa mengine.

Ripoti ya kutathmini athari za mazingira ambayo iliwasilishwa kwa NEMA miezi miwili iliyopita, ilionyesha kuwa, hoteli hiyo itajengwa kwa gharama ya karibu Sh515.8 milioni.

Ardhi itakayotumiwa kwa ujenzi huo iko karibu mita 100 kutoka ufuoni.

Hoteli hiyo ya kifahari itajengwa kwenye ardhi ambayo awali ilizozaniwa kati ya kampuni ya Kango na raia wa Uingereza John Unsworth.

Mnamo Agosti 5, mwaka uliopita, Jaji Millicent Odeny, alitoa uamuzi kwamba kampuni hiyo ndiye mmiliki halali, na kutaka jamaa wa Unsworth ambaye alishafariki wahame.

 

  • Tags

You can share this post!

Mackenzie sasa aamua heri kufa kuliko kuishi jela

Hofu ajira kupotea SGR ikifika Uganda

T L