• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Mackenzie sasa aamua heri kufa kuliko kuishi jela

Mackenzie sasa aamua heri kufa kuliko kuishi jela

NA BRIAN OCHARO

MSHUKIWA mkuu wa mauaji ya Shakahola, Bw Paul Mackenzie, sasa anasema yuko tayari kufa kuliko kuendelea kuteseka gerezani.

Bw Mackenzie aliilalamikia Mahakama ya Shanzu kuwa, anapitia mateso gerezani kwa kufungiwa kwenye chumba chenye giza kwa siku mbili bila kupata chakula wala kupata nafasi ya kuoga.

Alimwambia Hakimu Mkuu Mwandamizi Yusuf Shikanda kuwa, majaribio yake ya kutafuta usaidizi kutoka kwa wakubwa wa gereza hayajazaa matunda.

Kulingana naye, wasimamizi wakuu katika gereza hilo wanaonekana kukubaliana jinsi ya kumdhulumu.

“Mimi na wenzangu tumefanya uamuzi. Ukiona umenichoka mimi na wenzangu, tuko tayari kupelekwa Mto Yala. Hatuna shida na hilo kwa sababu nitakufa, na wewe kiongozi wa mashtaka siku moja utakufa kama mimi. Hakuna mahali utajificha,” alisema Mackenzie na kuongeza kuwa hajafungua kanisa lolote ndani ya gereza hilo.

Mackenzie alisisitiza katika ombi lake kwa mahakama kwamba halalamikii mateso hayo ili apate uhuru, bali ili mahakama iingilie kati na kumwokoa kutoka kwa dhiki anayopitia.

“Ninazuiliwa kwenye chumba chenye giza, na ombi langu la angalau saa moja kwenye jua limekataliwa kabisa. Ninahisi kutosikilizwa na kupuuzwa, na sina uhakika ni wapi pengine au ni nani ninaweza kutafuta msaada wake. Siwezi kutafuta msaada kwa upande wa mashtaka kwani watanikataa kwa sababu wananiona nina itikadi kali,” akasema.

Zaidi ya hayo, Bw Mackenzie, kupitia kwa wakili wake Wycliffe Makasembo, ameelezea wasiwasi kuhusu ukiukaji wa haki, kutengwa na ubaguzi.

“Mackenzie anapewa milo maalumu ambayo anahofia kuwa inaweza kutiwa sumu kwa nia ya kumdhuru. Hapo awali, washukiwa wote walikuwa wanakula pamoja lakini alitengwa na sasa anapewa chakula maalumu peke yake,” alisema wakili huyo.

Bw Mackenzie na washukiwa wenzake wametishia kugoma kula tena iwapo mateso hayo yataendelea.

“Watu hawa wakigoma kula tena, upande wa mashtaka utalaumiwa. Niliwasihi wawe watu wema, wakanisikia, lakini ni bahati mbaya kwamba upande wa mashtaka unataka kuturudisha tulipoanzia,” alisema Bw Makasembo.

Serikali iliomba siku nyingine 47 kuwazuilia, ikisema kuwa itakuwa mapema kuwafungulia mashtaka kabla ya kukamilisha uchunguzi wa mauaji ya Shakahola.

Serikali pia inasubiri uchunguzi wa DNA na wa kitaalamu ili kuthibitisha uhusiano wa kifamilia kati ya marehemu na washukiwa kabla ya kufungulia mashtaka.

 

  • Tags

You can share this post!

Ruto atetea kuzindua miradi ya serikali zilizopita kama...

NEMA yataka maoni yatolewe kuhusu ujenzi wa hoteli ya Raila

T L