• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
‘NYS haijatwaa usimamizi wa Kemsa’

‘NYS haijatwaa usimamizi wa Kemsa’

PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) Matilda Sakwa amepuuzilia mbali madai kuwa shirika hilo limetwaa usimamizi wa Mamlaka ya Dawa Nchini (Kemsa).

“NYS imeipiga jeki Kemsa jinsi ambavyo imekuwa ikifanya kwa idara nyingine za serikali. Kimsingi, NYS iko tayari kusaidia asasi yoyote ya serikali inayohitaji huduma zake. Hii haimaanishi kuwa NYS imetwaa usimamizi wa Kemsa. Kemsa inasalia Kemsa,” akasema Jumamosi katika chuo cha nyanjani cha NYS kilichoko Yatta, Machakos.

Bi Sakwa alikuwa mgeni wa heshima katika michezo baina ya vikosi 22 vya NYS kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi hayo alisema hayo kufuatia malalamishi yaliyoibuliwa kufuatia habari kwamba maafisa wa NYS wametumwa katika Kemsa kutekeleza majukumu ya wafanyakazi 600 waliopewa likizo ya mwezi mmoja.

Wakosoaji wa hatua hiyo, iliyosemekana kuchukuliwa na bodi ya Kemsa chini ya uenyekiti wa Bi Chao Mwadime, walisema wahudumu wa NYS hawajahitimu kuendesha kazi za kimatibabu.

Wengine walisema kuwa shirika la NYS limezongwa na madai ya ufisadi na hivyo haliwezi kuaminiwa kuendesha shughuli za Kemsa.

Lakini Seneta wa Narok Ledama Olekina, Alhamisi aliwaambia wanahabari katika Majengo ya Bunge, Nairobi, kwamba kuna njama ya kuiweka Kemsa chini ya usimamizi wa Jeshi la Kenya (KDF).

“Hatua hii ni kinyume cha sheria na sehemu ya mpango mpana wa serikali kuweka asasi ya umma chini ya usimamizi wa wanajeshi,” akasema Seneta Olekina.

Mwanasiasa huyo pia alipinga hatua ya kutumwa wafanyakazi 600 kwa likizo ya lazima kwa nia ya kuwafuta kazi akisema hatua hiyo ni kinyume cha haki za kimsingi za wafanyakazi hao.

“Iweje kwamba wakuu wa Kemsa waliohusika katika sakata ya wizi wa Sh7.8 bilioni pesa za umma wanaendelea kupokea nusu ya mishahara yao ilhali wafanyakazi wasio na hatia wanataka kufutwa? Hii sio haki na nitaipinga mahakamani ikiwa wabunge hawataizima,” Bw Olekina akasema, akionekana mwingi wa hasira.

Kamati ya Bunge kuhusu Afya pia imepinga mpango wa kuachishwa kazi kwa wafanyakazi wa ngazi za chini katika Kemsa.

Akiongea katika mkutano wa mashauriano na wadau katika sekta ya afya katika mkahawa mmoja Mombasa, Ijumaa, mwenyekiti wa kamati hiyo Sabina Chege aliahidi kuwa kamati yake itaita bodi ya Kemsa kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

You can share this post!

Chelsea wakabwa koo na Burnley katika EPL ugani Stamford...

Uhuru aliwapuuza waliotaka nishtakiwe kwa kosa la uhaini...

T L