• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
PK Salasya alia baada ya ‘kulemewa’ na bei ya viatu nchini Afrika Kusini

PK Salasya alia baada ya ‘kulemewa’ na bei ya viatu nchini Afrika Kusini

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Mumias Mashariki Peter Salasya amesema kuwa bei za bidhaa nchini Kenya ni nafuu kuliko nchi nyingine ambazo amewahi kuzuru.

Kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya X (zamani ikijulikana kama Twitter) Bw Salasya alitoa mfano wa jozi ya kiatu alivyokuwa amevalia akisema inagharimu Sh9,000 nchini Afrika Kusini ilhali Kenya bei ya jozi aina hiyo ni Sh5,000.

“Japo nchi ya Afrika Kusini imeendelea, maisha ni ghali. Hivi vyatu nilivyovaa vinagharimu Sh5,000 nyumbani Kenya ilhali hapa bei yake ni Rand 900 kiasi sawa na Sh9,000,” Bw Salasya akasema.

Mbunge huyo aliyechaguliwa bungeni kwa tiketi ya chama cha DAP-Kenya alisema kuwa amezuru nchi mbalimbali Afrika lakini amegundua kuwa gharama ya maisha nchini Kenya ingali chini.

“Kenya ni nchi nzuri ya kuishi. Changamoto inayowaumiza wananchi ni bei ya mafuta. Ikiwa bei ya mafuta itapunguzwa hakuna atakayetaka kuondoka Kenya kuenda kusaka maisha mazuri ng’ambo,” Bw Salasya akaeleza.

Mbunge huyo aliitaka serikali kupunguza bei ya mafuta ili Kenya iwe nchi nzuri ya kuishi. Bw Salasya alisema amezuru nchi za Afrika kama vile Sudan Kusini, Ghana, Tanzania, Morocco na sasa Afrika Kusini.

“Nawaomba Wakenya kupenda Kenya kwa sababu ni pahala pazuri pa kuishi,” Bw Salasya akasema.

Mnamo Oktoba 14, 2023, Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (EPRA) iliongeza bei ya petroli, dizeli na mafuta taa kwa wastani wa Sh5 kwa lita moja.

Hatua hiyo ilichangia bei ya petroli kupanda kutoka Sh212.06 hadi Sh217.36, dizeli hadi Sh205.47 kwa lita huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh205.06 jijini Nairobi na maeneo ya karibu.

  • Tags

You can share this post!

Ubomoaji wakamilika wahasiriwa wakienda hospitalini...

Ziara 38 ndani ya mwaka mmoja!

T L