• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Polisi 37 walikufa kazini ndani ya mwaka mmoja- ripoti yaonyesha

Polisi 37 walikufa kazini ndani ya mwaka mmoja- ripoti yaonyesha

NA CHARLES WASONGA

JUMLA ya maafisa wa 37 wa usalama walikufa wakiwa kazini ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kulingana na ripoti ya hivi punde kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani.

Kulingana na ripoti hiyo iliyotolewa Alhamisi Desemba 14, 2023 maafisa hao wanaotoka vikosi vya polisi wa kawaida, polisi wa utawala (AP), idara ya magereza na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walikufa kati ya Novemba 22, 2022 na Novemba 23, 2023.

Kati ya maafisa hao 37, 24 wanatoka Huduma ya Polisi Nchini (NPS), 10 wanatoka kitengo cha Huduma za Polisi wa Utawala, wawili wanatoka Huduma ya Magereza Nchini na mmoja anatoka idara ya DCI.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki aliwaongoza maafisa kutoka vikosi hivyo katika Ibada ya Pamoja ya Ukumbusho wa maafisa hao waliopoteza maisha yao wakiwa kazini.

Hafla hiyo ilifanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi wa Utawala, Embakasi, Nairobi.

Aidha, hafla hiyo pia ilihudhuriwa na familia za marehemu.

Idadi kubwa ya maafisa wa polisi wameuawa au kujeruhiwa wakiwa katika harakati za kupambana na wahalifu.

Maisha yao haswa yamo hatarini zaidi katika kaunti zilizoko Kaskazini Mashariki mwa Kenya kama vile Mandera, Wajir na Mandera zinazozongwa na mashambulio ya kila mara ya wanamgambo wa Al-Shabaab.

Kumekuwa na visa vya maafisa wa usalama kuuawa baada ya magari yao kulipuliwa na vilipuzi vilivyotegwa ardhini (IED) katika kaunti hizo zinazokaribiana na mpaka wa Kenya na Somalia.

Agosti 2023, Waziri Kindiki aliiambia Kamati ya Bunge kuhusu Usalama kwamba jumla ya maafisa 58 waliuawa na wahalifu wakiwa kazini tangu 2018.

Mnamo Novemba 10, 2012 jumla ya maafisa 42 wa polisi waliuawa wakati mmoja walipokuwa wakiendesha operesheni ya kupambana na majangili katika bonde la Suguta lililoko eneo la Baragoi, Kaunti ya Samburu.

Desemba, 2022 Waziri Kindiki alitangaza kuanzishwa kwa Hazina Maalum ya kusaidia familia za maafisa wa polisi na wale wa magereza waliokufa kazini.

“Hazina hiyo inatarajiwa kukusanya pesa za kusaidia familia zilizofiwa kwa kulipia watoto wao karo, kugharamia huduma za afya miongoni mwa mahitaji mengine,” Profesa Kindiki akasema mnamo Desemba 15, 2022.

Kimsingi, maafisa wa polisi huuawa na magaidi, majangili, wezi wa kimabavu, wenzao na hata raia.

Hata hivyo, rekodi za polisi zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya maafisa hao huuawa kwa kushambuliwa na majangili, haswa katika maeneo ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

 

  • Tags

You can share this post!

Sakaja azindua Kituo cha Huduma kwa Wateja

ODM yakana madai inagura Azimio

T L