• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Polisi waruhusu kufanyika kwa mkutano wa Raila uwanjani Kamukunji

Polisi waruhusu kufanyika kwa mkutano wa Raila uwanjani Kamukunji

JUSTUS OCHIENG, LEONARD ONYANGO NA MARY WAMBUI

MAAFISA wa Polisi wameruhusu muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya kufanya mkutano katika uwanja wa Kamukunji mchana wa leo Jumanne, amethibitisha mkuu wa polisi Nairobi Adamson Bungei.

“Walifanya matayarisho ya kutosha na kutafuta idhini kwa kufuata utaratibu,” Bw Bungei ameambia Taifa Leo.

Mkutano huo unaanza mchana huu mara tu Raila Odinga akitua kutoka nchini Poland.

Bw Odinga anatarajiwa kuongoza mkutano wa kisiasa ambapo atatangaza mapambano mapya dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.

Kulingana na Msemaji wa Bw Odinga, Dennis Onyango, kinara wa Upinzani ataelekea uwanjani Kamukunji, Nairobi, kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Kabla ya kuhutubia mkutano wa kisiasa Kamukunji, Bw Odinga atafanya kikao cha faragha na vinara wenzake wa Azimio uwanjani JKIA, kwa mujibu wa Bw Onyango.

Naibu kiongozi wa Azimio Martha Karua wiki iliyopita alitangaza kuwa Upinzani utaanda mkutano wa mashauriano na wananchi kabla ya kutoa mwelekeo kuhusu hatua inayofuatia.

Bw Odinga huenda akatangaza maandamano kama njia mojawapo ya kushinikiza serikali ya Kenya Kwanza kupunguza gharama ya maisha.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Bw Odinga amepata nguvu zaidi baada ya Rais William Ruto jana kutia saini Mswada wa Fedha wa 2023 kuwa sheria.

Bw Odinga analenga kutumia ushuru wa juu wa bidhaa na huduma mbalimbali kwenye Sheria ya Fedha kuhimiza wananchi kujiunga na maandamano ya Upinzani dhidi ya serikali.

Bw Odinga alisitisha maandamano yaliyokuwa yakifanyika kila Jumatatu na Alhamisi mnamo Aprili kupisha mazungumzo na serikali.

Sambaratika

Lakini mazungumzo hayo tayari yamesambaratika na upande wa Azimio umekuwa ukishutumu upande wa serikali kwa kuwachezea shere.

Kabla ya kusitisha maandamano kupisha mazungumzo, Bw Odinga alitumia mbinu mbalimbali kama vile kuhimiza wafuasi wake kususia bidhaa na huduma za baadhi ya kampuni alizodai kuwa rafiki kwa serikali, kuandikia barua Mahakama ya Kimataifa kuhusu Jinai (ICC) na kuunda Vuguvugu la Kupigania Demokrasia (MDD).

Mbinu hizo zote zinaonekana kugonga mwamba huku Rais Ruto akionekana kumlemaza kwa kuvutia upande wake baadhi ya wabunge wa Azimio.

Jana Jumatatu, Mbunge Maalumu John Mbadi alikanusha madai kwamba Bw Odinga anapanga kutangaza tena marufuku ya kususia bidhaa na huduma za baadhi ya kampuni.

“Kiongozi wa Azimio atatangaza mbinu mpya za kukabiliana na serikali leo,” akasema Bw Mbadi.

Bw Odinga amekuwa akishinikiza Rais Ruto kupunguza gharama ya vyakula na kufunguliwa kwa hifadhi ya matokeo ya urais akidai kwamba aliibuka mshindi katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Bw Odinga anataka kilo mbili za unga wa mahindi kuuzwa kwa chini ya Sh100 tofauti na sasa ambapo zinauzwa kwa Sh240.

Bw Odinga, wiki iliyopita aliibua mapambano mapya ambapo alimtaka Rais Ruto kuelezea Wakenya matumizi ya Sh213.4 bilioni alizodai zilikopwa na serikali kutoka kwa benki za humu nchini wiki mbili kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha Juni 30.

  • Tags

You can share this post!

Kamati maalum yaundwa kusuluhisha mzozo kuhusu matumizi ya...

Jinsi mamluki wa Wagner walivyosababisha kiwewe

T L