• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:21 PM
Jinsi mamluki wa Wagner walivyosababisha kiwewe

Jinsi mamluki wa Wagner walivyosababisha kiwewe

CHARLES WASONGA Na MASHIRIKA

UJASIRI wa kundi la Wagner wa kutaka kudhibiti ngome za wanajeshi nchini Urusi mnamo Jumamosi ulitishia uthabiti nchini humo na kuibua hisia mseto kote ulimwenguni.

Hii ni licha ya hakikisho kutoka kwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi Sergey Lavrov aliyesema kwamba “kila kitu kiko shwari Urusi.”

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya Alfred Mutua mnamo Jumamosi alizungumza na Lavrov na kumwelezea kuhusu “hofu ya Kenya kuhusiana na mashambulio yaliyotekelezwa na mamluki wa Wagner.”

“Nimeongea na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Urusi Sergey Lavrov kuhusiana na habari za mashambulizi yanayotekelezwa na kundi moja la mamluki. Amenijuza kuhusu hali nchini humo na kunihakikishia kuwa serikali ya Urusi inadhibiti hali na kila kitu kiko sawa. Nimemweleza kuhusu hofu na matarajio yetu,” Dkt Mutua akasema kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya Twitter.

Rais wa Urusi Vladimir Putin mnamo Jumamosi alielezea juhudi za kundi la Wagner la kuondoa mamlakani viongozi wa kijeshi wa Urusi kama “tishio kubwa kwa Urusi” na kutoa wito kwa raia kudumisha umoja.

“Machafuko yoyote ya ndani ni tishio kwetu kama taifa. Hili ni pigo kwa watu wetu,” Putin akasema kwenye taarifa iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya kitaifa ya Urusi.

Akaongeza: “Vita hivi, wakati hatima ya watu wetu inaamuliwa, vinahitaji umoja wa vikosi vyote vya kijeshi na umoja wa raia.”

Rais huyo aliungama Jumamosi kwamba “hali ngumu” ilishuhudiwa katika jiji la Rostov-on-Don lililoko kusini mwa Urusi ambako kundi la Wagner lilitwaa udhibiti wa vituo vikuu vya kijeshi katika jitihada zao za kung’oa mamlakani wakuu wa wanajeshi hao.

“Hatua madhubuti zitachukuliwa kuleta uthabiti jijini Rostov-on-Don,” Putin akasema.

Mnamo Juni 25, mamluki wa Wagner walirudi kwa kambi zao, baada ya Putin kumuepushia kiongozi wao Yevgeny Prigozhin uwezekano wa kufunguliwa mashtaka ya uhaini na kukubali akimbilie nchini Belarus.

Rais wa Belarus Alexander Lukashenko ambaye tokea mwanzo alisema alikuwa mstari wa mbele kuzima maasi hayo, amesema leo Jumanne, Juni 27, 2023 kwamba mgogoro baina ya wanajeshi wa Urusi na mamluki wa Wagner ambao umekuwepo kwa muda mrefu, haukushughulikiwa ipasavyo.

Mamluki hao ambao wamekuwa wakisaidia Urusi kupambana na Ukraine, wanadai kwamba jeshi la Urusi limekuwa likishambulia ngome zao ili kutokomeza kundi hilo.

  • Tags

You can share this post!

Polisi waruhusu kufanyika kwa mkutano wa Raila uwanjani...

Mkongwe Roy Hodgson kuendelea kudhibiti mikoba ya Crystal...

T L