• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Polisi wawinda majambazi waliomuua afisa wa DCI

Polisi wawinda majambazi waliomuua afisa wa DCI

NA SAMMY KIMATU

POLISI wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa cha afisa wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) ambaye inadaiwa aliuawa na majambazi alipokuwa akielekea nyumbani akiwa na mkewe katika eneo la Chokaa, kaunti ndogo ya Njiru.

Mkuu wa polisi katika eneo la Kayole, Bw Paul Wambugu amesema Ijumaa kwamba hakuna mshukiwa amekamatwa kufikia sasa.

Hata hivyo, amethibitisha kuwa mpelelezi bingwa wa chembechembe za DNA aliyeuawa, alikuwa akihudumu katika kituo cha polisi cha Industrial Area.

Akiongea na Taifa Leo, mkuu wa polisi eneo la Makadara Judith Nyongesa amethibitisha kuwa Bw David Mayaka Anyansa alikuwa afisa wa jinai katika divisheni ya Makadara tangu 2019.

“Ni huzuni kumpoteza afisa wetu aliyependa kazi yake. Alikuwa mpole na alikuwa ni mtu wa bidii,” Bi Nyongesa akasema.

Kwa mujibu wa naibu mkurugenzi wa upelelezi wa jinai Makadara, Inspekta mkuu Jared Seko, marehemu Bw Mayaka alikuwa mpelelezi aliyebobea katika masuala ya DNA.

Bw Seko alisema Mayaka, mzaliwa kutoka kaunti ya Nyamira, alisomea maswala ya DNA nchini India miongozi mwa nchi nyingine.

“Marehemu Bw Mayaka alichangia sana katika sekta ya upelelezi wa kutafuta matokeo ya chembechembe za damu (DNA) KatikaTaasisi ya Utafiti wa Afya Nchini (KEMRI) kwa muda mrefu,” Bw Seko askasema.

Siku ya kisa, kwa mujibu wa Bw Seko, gari la afisa huyo lilipata panjari. Alikuwa amelinunua siku tatu kabla ya kukutana na kifo chake katika eneo la Chokaa akiambatana na mkewe Hellen Kemunto mwendo wa saa tatu na nusu usiku huo wa Jumanne.

Katika harakati za kurudisha gurundumu lililotoboka ndipo majambazi watatu waliokuwa na pikipiki iliyofunikwa nambari za usajili waliwasili na kumpiga risasi pamoja na mkewe.

“Alikuwa amemaliza kubadilisha gurudumu la gari lake alipopigwa risasi tumboni na mkewe kufyatuliwa risasi pia kwenye paja lake la mguu wa kushoto. Walikimbizwa Komarock Hospital kabla ya kuhamishwa hadi Nairobi West ambapo Bw Mayaka alifariki,” Bw Seko akasema.

Vilevile ameongeza kwamba Bi Kemunto anaendelea vyema hospitalini baada ya madaktari kumshughulikia.

Amesema mseto wa timu ya maafisa wa upelelezi kutoka Makadara, Kayole na kanda ya Nairobi wako mbioni kuwasaka wahalifu waliohusika na tukio hilo.

Kadhalika, Bw Seko amekiri kwamba tukio hilo ni la kipelee na la kwanza kushuhudiwa katika divisheni ya Makadara.

“Naweza kufananisha kisa hiki na kingine kilichotokea Kasarani wakati afisa wetu aliuawa katika makabiliano makali ya risasi kati ya polisi na majambazi kabla ya majambazi hatimaye kuuawa kwa mtutu wa bunduki,” Bw Seko akasimulia.

  • Tags

You can share this post!

Mashabiki wa kandanda Lamu waipa Manchester City kichwa

Hospitali, daktari kumlipa mwanamke fidia ya Sh1.1 milioni...

T L