• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
Mashabiki wa kandanda Lamu waipa Manchester City kichwa

Mashabiki wa kandanda Lamu waipa Manchester City kichwa

NA KALUME KAZUNGU

MASHABIKI wa soka kisiwani Lamu wamesema wanatarajia mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kati ya Manchester City na Burnley leo usiku katika uwanja wa Turf Moor itaisha kwa mabao 3-0 kwa faida ya wageni.

Licha ya mashabiki hao kuwa wa klabu tofauti tofauti za EPL, zikiwemo Manchester United, Arsenal, na Chelsea miongoni mwa timu nyingine, wanakiri kwamba mechi ya leo kwa Manchester City ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo, ni mteremko kwao.

Wanadai Burnley ni makinda kwa klabu ya Manchester City ambayo wameitaja kuwa na uzoefu mkubwa ligini.

Said Hashim, almaarufu DJ Fakhrudin, anasema usajili mpya ambao kocha wa Manchester City Pep Guardiola alifanya msimu huu wa 2023/2024 ni wa nguvu si haba na kwamba kamwe Burnley hawatatamba mbele ya mibabe hao.

Mechi hiyo itaanza majira ya saa mbili usiku.

“Mimi ni shabiki kindakindaki wa Manchester United lakini kusema kweli Mgala muue na haki yake umpe. Hawa Manchester City leo watatandika Burnley mabao 3-0. Twawavulia kofia kwa weledi wao wa soka,” akasema Bw Hashim.

Ibrahim Lali ambaye ni shabiki wa Arsenal pia amekubali kuwa ushindi wa mechi ya leo utaendea Manchester City, akiitaja Burnley kuwa klabu changa ligini.

Bw Lali hata hivyo ametoa onyo kwa mibabe Manchester City kwamba kiboko chao msimu huu ni Arsenal.

“Leo nakubali ushindi utatwaliwa na Manchester City lakini wafahamu kabisa kwamba chuma chao ni Arsenal. Tumejiandaa vilivyo msimu huu wa 2023/2024 na lazima tuwafunze mpira hawa Man City,” akasema Bw Lali.

Kalu Jefwa, shabiki wa Chelsea anasema Manchester City leo watatandika Burnley 3-1 matokeo ambayo anatabiri yatakuwa sawa sawa na Chelsea watakaoadhibu mahasimu wao Arsenal kwenye ngarambe itakayochezwa ugani Emirates mnamo Jumapili.

Jefwa Kalu, shabiki wa Chelsea kisiwani Lamu. Asema Manchester City watatandika Burnely mabao 3-1.
PICHA | KALUME KAZUNGU

Douglas Wasike, shabiki wa Manchester United alitaja sajili mpya za Manchester City msimu huu kama vile Jasko Gvardiol kuwa wachezaji walioongeza moto safu ya mabingwa hao watetezi.

Bw Wasike aidha alitaja klabu ya Manchester United, Arsenal na Chelsea kwamba zitazidisha ladha ya mechi za EPL msimu huu kutokana na jinsi zilivyojiandaa kikamilifu kuona kwamba zinatwaa ligi baada ya kipindi kirefu cha ukame wa makombe.

“Klabu hizo tatu ukitazama sajili zao mpya mwaka huu ni za kuridhisha si haba. Pia zimejiandaa kikamilifu kuona kwamba zinatwaa ubabe wa EPL,” akasema Bw Wasike.

Manchester City, chini ya mkufunzi Pep Guardiola, wako chonjo kuona kwamba wanahifadhi hadhi yao ya kuitawala ligi ya EPL.

Kwa upande wao, Burnley, chini ya mkufunzi wao raia wa Ubelgiji, Vincent Kompany, ambaye pia zamani aliichezea Manchester City, nao wako mbioni kuona kwamba wanaandikisha matokeo bora kwenye ligi ya EPL baada ya kupandishwa ngazi msimu huu wa 2023/2024.

  • Tags

You can share this post!

Limbukeni Shanderema walipuliwa na St Anthony’s

Polisi wawinda majambazi waliomuua afisa wa DCI

T L