• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Raila amtaka Ruto kushusha bei ya mafuta ya petroli kwa Sh50   

Raila amtaka Ruto kushusha bei ya mafuta ya petroli kwa Sh50  

STANLEY NGOTHO na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, sasa anaitaka serikali ya Kenya Kwanza kupunguza bei ya mafuta ya magari kwa kima cha Sh50.

Akiongea Jumamosi, Desemba 9, 2023 katika Kaunti ya Kajiado, Bw Odinga alitaja kushuka kwa bei mafuta katika masoko ya ulimwengu kama sababu ya kuitaka serikali kushusha bei ili kuwapa raia afueni.

Kwa mara nyingi, alimsuta Rais William Ruto kwa kuendesha serikali isiyojali maslahi ya wananchi kwa kuwatoza ushuru wa juu na kudinda kupunguza gharama ya maisha.

“Tunafahamu fika kwamba bei ya mafuta katika masoko ya ulimwengu imepungua kwa kiwango kikubwa. Kwa hivyo, tunataka bei ya bidhaa hiyo nchini kushuka mara moja. Bei isipunguzwe kwa Sh5 tu kuwahadaa Wakenya, bali kwa kiwango cha kuanzia Sh48 hadi Sh50,” Bw Odinga akasema.

Alikuwa akizungumza katika kijiji cha Merrueshi, eneo bunge la Kajiado Mashariki, ambako alihudhuria hafla ya kutoa shukrani kwa heshima ya Mbunge wa eneo hilo Kakuta Maimai.

Mbunge huyo, anayehudumu bungeni kwa muhula wa kwanza, alichaguliwa kwa tikiti ya ODM.

Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Petroli (EPRA) hutumia viwango vya bei ya mafuta katika masoko ya ulimwengu kukadiria bei mpya ya rejareja ya bidhaa hiyo tarehe 14 kila mwezi.

Mnamo Alhamisi, Desemba 7, 2023 bei ya bidhaa hiyo ilishuka hadi dola 69.6 (sawa na Sh10,676.28) kwa pipa – bareli katika masoko ya kimataifa.

Bei hiyo ya mafuta yasiyosafishwa kutoka kampuni ya Murban, ni ya chini zaidi kushuhudiwa tangu Julai mwaka huu, 2023, japo ilikuwa juu kidogo kuliko bei ya Jumatano, Desemba 6.

Juni 2023 bei hiyo ilishuka hadi dola 69.15 ya Amerika, sawa na Sh10,607.73 kwa pipa.

Novemba 14, EPRA iliweka bei ya mafuta aina ya petroli katika kiwango cha Sh217.36 kwa lita, huku dizeli ikiwa Sh203.47 jijini Nairobi.

Bw Odinga pia aliishutumu serikali kutokana na mipango yake ya kuuza mashirika 11 ya umma, yenye thamani Sh200 bilioni.

  • Tags

You can share this post!

Kinara wa Benki ya Equity na familia ya Moi wakabana koo...

Raia wa Uholanzi motoni kwa kudhulumu watoto kingono

T L