• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 7:55 AM
Raila atema washauri wa jadi, ateua wapya

Raila atema washauri wa jadi, ateua wapya

Na LEONARD ONYANGO

KINARA wa ODM, Raila Odinga amewatema baadhi ya washauri wake alioshirikiana nao kwa karibu kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, na badala yake kukumbatia wandani wa Rais Uhuru Kenyatta akijiandaa kuwania urais mwaka ujao.

Miongoni mwa washauri ambao Bw Odinga ameonekana kujitenga nao ni Seneta wa Siaya James Orengo, mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, msomi wa Sayansi ya Siasa na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi Prof Adams Oloo na mfanyabiashara Jimi Wanjigi.

Bw Orengo amekuwa mshauri wa masuala ya siasa wa Bw Odinga kwa miaka mingi lakini ameonekana kukaa mbali tangu kinara wa ODM alipotangaza kushirikiana na Rais Kenyatta, almaarufu handisheki, mnamo 2018.Bw Orengo na Dkt Amollo walikuwa miongoni mwa washauri waliomshawishi Bw Odinga kususia kura za mararudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017 kwa madai Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilipendelea Rais Kenyatta wa Jubilee.

Bw Orengo amekuwa akitumia muda mwingi kusaka kura za ugavana wa Siaya. Naye Dkt Amollo ameanza kampeni za kutetea kiti chake cha ubunge wa Rarieda katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.Wawili hao wamekuwa wakisaka kura pamoja katika Kaunti ya Siaya na wamelegeza kamba katika siasa za kitaifa.

Mahojiano yaliyofanywa na Taifa Leo yamebaini kuwa, Bw Orengo huenda akawa miongoni mwa wanasiasa wa ODM ambao watapewa tiketi ya moja kwa moja.Katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017, Bw Orengo alikuwa kwenye mstari wa mbele kuendesha kampeni za kitaifa za Bw Odinga kiasi kwamba, alichaguliwa na wakazi wa Siaya bila kufanya kampeni yoyote.

“Hatua ya Raila kumtuma Bw Orengo kujihusisha na kampeni za kaunti ni ishara kwamba, hamhitaji katika ulingo wa siasa za kitaifa,” asema wakili Felix Otieno. Bw Wanjigi ambaye alikuwa kiungo muhimu katika kusaka fedha za kampeni za Bw Odinga 2017, sasa amegeuka mkosoaji wa sera za waziri mkuu huyo wa zamani licha ya kushikilia kwamba angali mwanachama wa ODM.

“Inaonekana Bw Odinga ameachana na washauri wake wenye msimamo mkali kama vile Bw Orengo.“Vilevile, anaonekana kupunguza washauri kutoka eneo la Nyanza ili kikosi chake kiwe na sura ya kitaifa kwa kuingiza wandani wa Rais Kenyatta,” anasema Bw Otieno.

Wakili Paul Mwangi ambaye amekuwa mshauri wa Bw Odinga kuhusu masuala ya siasa kwa miaka 10, ametwikwa jukumu la kuongoza kikosi cha mawakili watakaoshauri kinara wa ODM huku akiendelea na mikakati ya kuwania urais mwaka ujao.

Kiongozi wa ODM pia ameunda kikosi kipya cha washauri wa masuala ya uchumi kinachoongozwa na Prof Peter Wanyande, msomi na mtaalamu wa masuala ya siasa na uchumi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.Uchumi sasa ni suala kuu ambalo litatawala kampeni za urais za Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Kikosi hicho kimechukua mahala pa mwanauchumi Dkt David Ndii ambaye amehamia kambi ya Naibu wa Rais William Ruto.Washauri wengine wa sasa wa Bw Odinga ni Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, Mshauri wa Rais Kenyatta kuhusu masuala ya siasa Mutahi Ngunyi, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Kisiasa (Cotu) Francis Atwoli, mmiliki wa shirika la habari la Royal Media Samuel Macharia na kundi la mabwanyenye wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF).

Washauri wa kisiasa wa Bw Odinga ni magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Hassan Joho (Mombasa), Dkt James Nyoro (Kiambu), Ndiritu Muriithi (Laikipia), Bw Francis Kimemia (Nyandarua) .

You can share this post!

Duale aapa kupinga Mswada wa miungano ya kisiasa

Maandalizi ya kisasa kwa Team Kenya Jumuiya ya Madola

T L