• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Rais Ruto azindua pikipiki za umeme mjini Mombasa

Rais Ruto azindua pikipiki za umeme mjini Mombasa

NA JURGEN NAMBEKA

HUENDA waendeshaji wa bodaboda nchini wakawezeshwa kuendesha shughuli za uchukuzi kwa gharama ya chini zaidi, baada ya Rais William Ruto kuzindua bodaboda za umeme, alizokuwa amewaahidi Wakenya miezi mitatu iliyopita.

Rais Ruto alizindua pikipiki hizo katika bustani ya Mama Ngina jijini Mombasa, akitaja kama hatua itakayowafaidi wahudumu wa bodaboda.

Kulingana naye, kando na kutoa nafasi za ajira kwa vijana, mchakato wa kuhamia kwa usafiri wa umeme, utaiwezesha taifa la Kenya kukabiliana ipaswavyo na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

“Tutakuwa na kongamano la kujadili sera za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kuanzia Jumatatu. Ili tuweze kuwa mstari wa mbele kupunguza kiwango cha kaboni inayoachiliwa hewani, ni lazima tuafnye mabadiliko katika sekta ya usafiri na haswa bodaboda ambayo ina zaidi ya piki piki milioni moja,” akasema Dkt Ruto.

Pikipiki hizo zimeundwa na kampuni ya Spiro, na zinauzwa kwa mkopo kwa kima cha Sh 190,000.

Na wale wenye uwezo wa kununua kwa pesa taslimu watazipata kwa Sh 160,000.

Kulingana na rais Ruto, hatua ya kupunguza ushuru wa vifaa vya kutengeneza vyombo vya usafiri vya umeme, kulipunguza bei ya pikipiki hiyo ambayo ingepaswa kuuzwa kwa Sh 300,000.

“Ndani ya miezi sita nataka washirika wetu Spiro waweze kuunganisha pikipiki hizi katika kampuni yao kule Dongo Kundu, Na ndani ya mwaka mmoja, wawe na uwezo wa kuitengenezea hapa. Haya yakifanyika bei hiyo itapunguka zaidi,” akasema rais Ruto.

Rais alieleza kuwa baada ya kuhamia kikamilifu kwa usafiri wa kielektoniki wa pikipiki, serikali yake itaanza kuzuia kuingizwa nchini kwa pikipiki za petrol.

Alieleza kuwa kwa watakao pata pikipiki hizo kwa mkopo, Sh236 itakatwa kila siku kwenye akaunti zao za Mpesa.Na kubadilisha betri katika vituo vya kubadilishia mbalimbali, kutatozwa Sh 220.

“Kwa Sh 500 pekee yake, watu wangu wa bodaboda mtaweza kuendesha pikipiki zenyu kwa umbali wa kilomita 70. Pikipiki hizi ni za bei nafuu hata kushinda bodaboda zinazotumia petroli,” akasema Dkt Ruto.

Kulingana na Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen, ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria uzinduzi huo, bodaboda hizo zitaisaidia serikali kudumisha nidhamu barabarani.

Bw Murkomen alieleza kuwa bodaboda hizo zimewekewa vidhibiti mwendo.

“Tumepoteza zaidi ya Wakenya 5000 katika ajali za barabarani. Cha kusikitisha ni kuwa vifo 3000 vinahusihwa na bodaboda. Hii boda boda ya ielektroniki haiwezi kuenda zaidi ya kilomita 70 kwa kila saa. Itatusaidia kupambana na waendeshaji wasio na nidhamu,” akasema Bw Murkomen.

Waziri Murkomen alieleza kuwa wizara yake imeteua jopokazi la kuandaa sera za matumizi ya vifaa vya usafiri vya kielekroniki humu nchini.

Kwa upande wake, Gavana wa Mombasa Abdulswammad Nassir, ambaye pia alihudhuria uzinduzi huo, aliahidi kununua angalau bodaboda 12 atakazogawa kwa makundi ya vijana wa maeneobunge ya kaunti yake.

Kulingana naye, kuzinduliwa kwa mradi huo Mombasa, kulikuwa ishara kuwa vijana wa Mombasa walipaswa kuwa wa kwanza kukumbatia usafiri wa kielekroniki.

“Serikali yangu iko tayari kuhakikisha hata wafanyakazi wa kaunti wanahamia kwa usafiri wa kielektroniki. Kwa hivyo kwa Saccos sita za hapa Mombasa, nitawapa piki piki ili tuwe wa kwanza katika safari hiyo,” akasema Bw Nassir.

 

  • Tags

You can share this post!

Kisanga polo akilaumu kahaba kwa kumzima nguvu za kiume...

Wazee Mlima Kenya wataka waruhusiwe kutembea na visu,...

T L