• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Wazee Mlima Kenya wataka waruhusiwe kutembea na visu, marungu

Wazee Mlima Kenya wataka waruhusiwe kutembea na visu, marungu

NA MWANGI MUIRURI

WAZEE wa Gikuyu, Embu na Meru (Gema) sasa wanaitaka serikali ikome kuharamisha ubebaji wa silaha za kitamaduni miongoni mwa wanaume wa eneo hilo.

Wakiongea katika Mkahawa wa Southern Blue, Jumamosi ya Septemba 2, 2023, wazee hao walisema Usalama wa boma na mali Mlima Kenya umefanyiwa mzaha hata na serikali yenyewe.

Wakiongozwa na Mzee Joseph Kaguthi ambaye alihudumu kama mkuu wa mkoa tangu hadi alipostaafu 1999 walisema kwamba wanaume wa eneo hilo wamelemazwa kukinga familia zao na mifugo dhidi ya wavamizi.

“Licha ya sheria ya kujihami kwa silaha za kitamaduni kufanyiwa marekebisho mwaka wa 1983 na kukubalia jamii kujihami kwa lengo la kujikinga athari za uvamizi, sisi Mlima Kenya tumeendelea kuchukuliwa kama majangili tukionekana hadharani na vifaa vya kivita,” akasema.

Bw Kaguthi alisema hali hiyo imelemaza jamii za Mlima Kenya katika harakati za kulinda mimea, mifugo na mali zingine dhidi ya wezi.

“Kwa sababu tunajulikana kwa kutokuwa na silaha za kijamii kama mishale, mikuki, mapanga na marungu, wavamizi hutushambulia kwa raha zao, hutuhangaisha na kutudunisha jinsi watakavyo,” akasema.

Bw Kaguthi alisema kwamba kwa sasa “kilio mashinani kwetu ni mimea kuibwa shambani, mifugo kutolewa zizini na hata sisi kushambuliwa na kuuawa kwa kuwa inajulikana vyema serikali imeharamisha uwezo wetu wa kujihami ili kujikinga,” akasema.

Mwenyekiti wa muungano wa Wazee wa Agikuyu Bw Wachira Kiago alisema kwamba “jamii nyingine zimepewa ruhusa ya kujihami kitamaduni hata baadhi zikipewa bunduki na serikali lakini sisi wenye mali na tulio katika hali ya kulengwa na wazi tukitakiwa tubakie bila uwezo wa kujikinga”.

Bw Kiago alisema “kujihami kwa silaha za kitamaduni kwa masilahi za kuimarisha Usalama wa boma sio hatia”.

Ajabu, akasema, jamii kama ya Maasai huonekana hata katika miji mikuu wakibeba simi, rungu, vijiti vilivyo na misumari, nyaunyo, mishale na mikuki na badala ya kukamatwa, serikali inawashamgilia huku ikiita wazungu waje umasaaini kushuhudia utamaduni.

“Lakini mtu wa Mlima Kenya akionekana hata na mkongojo wa kupiga jeki uzee miguuni, polisi wanaitwa wamfuatilie kujua yuko na nia gani. Huo ubaguzi ndio tunakataa kwa sasa,” akasema.

Mzee Ndung’u wa Ruhiu kutoka Nyeri alisema kwamba Naibu wa Rais Bw Rigathi Gachagua anafaa kushirikiana na Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki kutokomeza ubaguzi huo.

“Jamii za Mlima Kenya zimeumia sana mikononi mwa maadui kwa kuwa zimezimwa kujipa kinga dhidi ya uvamizi. Kwa boma, zizini, kwa biashara na hata kwa shamba tunatakiwa tushirikiane na wavamizi wakitushambulia na tubaki kulialia kwamba serikali saidia,” akasema.

Bw Zack Kinuthia ambaye alihudumu kama Naibu Waziri  kwa nyakati tofauti wa Spoti na pia Elimu katika utawala wa Rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba “sisi tukijihami tunahusishwa na kundi haramu la Mungiki lakini wengine wanasemwa kuwa wapenzi wa utamaduni”.

Alisema kwamba mwanamume wa Mlima Kenya hata anaweza akapokonywa bibi akiwa katika boma lake kwa kuwa akijaribu kutetea hadhi hata kwa kujihami na kigongo, atakamatwa na ashtakiwe kwa kuwa jambazi sugu.

“Ningetaka sasa ieleweke vyema na wanaume wote wa jamii yetu kwamba sio hatia kujihami kwa silaha za kitamaduni bora tu usitokee nazo barabarani kutekeleza vituko vya kusambaratisha amani,” akasema Mzee Kaguthi.

Kaguthi aliongeza kuwa “sio hatia kujikinga na pia kuwakinga majirani pamoja na mali yao dhidi ya majambazi kwa kutumia silaha hizo za kitamaduni”.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto azindua pikipiki za umeme mjini Mombasa

PENZI LA KIJANJA: Chali akikuvunja moyo mteme mara moja, la...

T L