• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Ruto: Nilichaguliwa kubadilisha maisha ya Wakenya, si kuwania muhula wa pili

Ruto: Nilichaguliwa kubadilisha maisha ya Wakenya, si kuwania muhula wa pili

NA SAMMY WAWERU

RAIS William Ruto amesuta vikali wanaomkosoa jinsi anavyoendesha nchi akisema alichaguliwa kubadilisha maisha ya Wakenya. 

Licha ya gharama ya maisha kuzidi kuongezeka na kulemea wananchi, Dkt Ruto amesema shabaha yake ni kuona Kenya imeimarika.

Alisema hajalishwi na vitisho vya wapinzani wake “ambapo wanasema nitahudumu muhula mmoja pekee”.

Akiwajibu Jumapili jioni, Desemba 17, 2023 kwenye mahojiano ya pamoja na vyombo vya habari, Dkt Ruto alisema hajalishwi endapo hatarejea tena.

“Ninaskia watu wakisema, eti ukiendelea vile tunaona, hutapata muhula wa pili. Ninawaambia; Sikuchaguliwa ili nihudumu muhula wa pili,” Rais alisema.

Mahojiano hayo yalipeperushwa moja kwa moja kupitia runinga kuu za habari nchini.

Aliongeza, “Nilichaguliwa kubadilisha Kenya”.

Kulingana na kiongozi wa nchi, serikali za awali zimekuwa zikiahirisha mambo na mikakati kukuza Kenya, ikiwa ni pamoja na kutathmini ushuru (VAT) na ada ya bidhaa kuongeza mapato ya serikali kuu ifanye maendeleo.

Chini ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita – tangu atwae mamlaka Septemba 2022, gharama ya maisha imepanda mara dufu hasa baada ya nyongeza ya VAT kwa bidhaa za mafuta ya petroli.

Serikali ya Kenya Kwanza, inayoongozwa na Ruto, ilipandisha ushuru wa petroli kutoka asilimia 8 hadi 16, hatua ambayo imechochea mfumko wa bei ya bidhaa muhimu za kimsingi.

“Hatutaendelea kuahirisha mambo. Kenya, hadhi yake ni sawa na mataifa kama Afrika Kusini, Morocco na Tunisia,” Rais Ruto aliambia wanahabari waliomhoji.

Akidai kwamba amesaidia kushusha gharama ya chakula kwa kiwango kikubwa, alipuuzilia mbali maombi ya viongozi wa kidini kumtaka asikilize kilio cha Wakenya na upinzani, akisema hatua aliochukua kuendesha nchi ina machungu ila baada ya muda, uchumi utaimarika.

“Ninachofanya ninajua Wakenya watanituza vizuri,” akaelezea.

Alitumia mfano wa uongozi wake kama ule wa Rais Mstaafu, Marehemu Mzee Mwai Kibaki, ambaye anaendelea kupigiwa upatu kutokana na jinsi aliboresha Kenya chini ya kipindi cha miaka kumi pekee.

 

  • Tags

You can share this post!

Fahamu kuhusu barabara nne zinazowatia hofu wakazi wa Lamu

Ruto akiri kuongoza nchi kama Rais si mteremko

T L