• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Ruto apata ‘nyaunyo’ kwa jina Felix Koskei kucharaza watundu serikalini

Ruto apata ‘nyaunyo’ kwa jina Felix Koskei kucharaza watundu serikalini

NA WANDERI KAMAU

MKUU wa Utumishi wa Umma, Bw Felix Koskei, ameibukia kuwa ‘mtu mpya wa mkono’ wa Rais William Ruto, kwa kutekeleza majukumu muhimu ambayo kikatiba yanafaa kutekelezwa na mawaziri wanaosimamia wizara zao.

Ijapokuwa kikatiba majukumu ya msingi la Mkuu wa Utumishi wa Umma yanafaa kuwa msaidizi wa Rais katika kusimamia Idara ya Utumishi wa Umma (PSC) na uendeshaji wa vikao vya Baraza la Mawaziri, mamlaka ya Bw Koskei yanaonekana kuzidi majukumu hayo mawili ya msingi.

Mnamo Alhamisi, Septemba 29, 2023, Bw Koskei alitoa onyo kwa polisi wafisadi, chini ya uwepo wa Inpekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome. Hatua hiyo ni licha ya Afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi kuwa huru.

“Ninatoa onyo kwa polisi ambao watapatikana wakichukua hongo. Jukumu lenu kuu ni kuwahudumia raia,” akasema Bw Koskei, alipowahutubia maafisa wa ngazi za juu katika Idara ya Polisi katika Taasisi ya Masuala ya Utawala (KSG), eneo la Kabete.

Mnamo Septemba 2023, Bw Koskei pia alionekana kuchukua mamlaka ya Waziri wa Maji, Bi Alice Wahome, kwa kuwaagiza maafisa wakuu watendaji wa Mamlaka ya Kusimamia Kazi za Maji ya Athi (AWWDA), Bw Michael Thuita, na mwenzake wa Mamlaka ya Kusimamia Kazi za Maji ya Kati mwa Bonde la Ufa (CRVWWA), Bw Samuel Oruma, kuondoka katika nyadhifa zao ili kutoa uchunguzi dhidi yao kufanywa kuhusu tuhuma za ufisadi.

Hatua hiyo ilikuwa kinyume na msimamo wa Bi Wahome, aliyeshikilia kuwa wawili hao walifaa tu kuondoka ofisini ikiwa uchunguzi utakaoendeshwa utawapata na hatia.

Kimsingi, Bw Koskei huchukua maagizo moja kwa moja kutoka kwa Rais; pia, huwa anasimamia Afisi ya Mawaziri ambayo hutoa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kwa Idara nyingine za serikali, husimamia utendakazi wa ushirikiano baina ya wizara na idara tofauti za serikali huku akidumisha ushirikiano baina ya idara hizo na umma.

Mnamo Juni, Bw Koskei alifanya kikao na wafanyakazi wa Mamlaka ya Kusambaza Dawa Kenya (KEMSA), ambapo alitoa onyo kali kwao dhidi ya kupatikana kuhusika katika sakata yoyote ya ufisadi.

Kwenye kikao hicho, Bw Koskei alitangaza mpango wa serikali kuwafuta kazi zaidi ya wafanyakazi 200 wa mamlaka hiyo, kwenye mkakati wa “kupunguza matumizi ya fedha za serikali katika kulipia mishahara ya wafanyazi”.

Kulingana na wadadisi, hilo ni jukumu linalofaa kutekelezwa na Waziri wa  Afya, Bi Susan Nakhumicha, ikizingatiwa idara hiyo iko chini ya wizara yake.

Kwenye kikao hicho, Bw Koskei pia alitangaza kuchukua mkakati kama huo “kulainisha idara zote za serikali ambazo haziwajibiki vilivyo”.

Mnamo Julai, Bw Koskei alizuru mradi wa serikali wa kilimo wa Galana-Kulalu, katika Kaunti ya Kilifi, ambapo alitangaza mikakati ambayo serikali itachukua katika kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

Ijapokuwa aliandamana na Katibu wa Idara ya Unyunyizaji, Ephantus Kimotho na Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Unyunyizaji (NIA), Bw Charles Muasya, maswali ambayo yaliibuka ni kwa nini Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi, hakuwepo kwenye ziara hiyo.

Kulingana na wadadisi, mchipuko wa ghafla wa Bw Koskei katika kile anataja kuwa “ulainishaji wa idara za serikali” unaonyesha nafasi kubwa aliyo nayo katika utawala wa Kenya Kwanza, na huenda pia ukaashiria kuwa Rais Ruto hawaamini baadhi ya mawaziri wake kusimamia idara muhimu.

Kwenye mahojiano na Taifa Jumapili, mdadisi wa siasa Oscar Plato anasema kuwa kikatiba, jukumu la Bw Koskei linafaa kuwaambia mawaziri katika idara husika masuala wanayofaa kutekeleza wala si yeye mwenyewe kuonekana kuyatekeleza.

“Katika tawala za hapo awali, hatujawahi kumwona Mkuu wa Utumishi wa Umma akiwa nyanjani, huku akitoa maagizo kwa wafanyakazi katika idara husika za serikali. Hilo huwa ni jukumu la mawaziri wanaosimamia wizara hizo,” akasema Bw Plato.

Kulingana naye, hatua ya Rais Ruto kumtuma kulainisha baadhi ya idara na kutowajumuisha mawaziri wanaohusika, inaashiria dalili za Rais kukosa imani na utendakazi wa baadhi ya mawaziri wake na kuongezeka kwa imani baina ya Rais Ruto na Bw Koskei.

“Ikiwa mwelekeo huo utashuhudiwa katika idara nyingine kama alivyoahidi Bw Koskei, basi ufasiri wa moja kwa moja utakaokuwepo ni kuwa yeye ndiye mtu mpya wa mkono anayeaminika zaidi na Rais kuliko mawaziri wake,” aeleza.

Ijapokuwa baadhi ya mawaziri wanasisitiza kuwa bado ni waandani wa karibu wa Rais, wadadisi wanaonya kuwa kupanda hadhi kwa Bw Koskei huenda kukaashiria dalili wa mwelekeo tofauti wa kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Abiria Nairobi walia kunguni kuwatafuna kwenye matatu

Masoko Nairobi na Kiambu yanayouzia wateja mbegu za avocado...

T L