• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Abiria Nairobi walia kunguni kuwatafuna kwenye matatu

Abiria Nairobi walia kunguni kuwatafuna kwenye matatu

NA RICHARD MAOSI.

ABIRIA wanaotumia magari ya umma (PSV) jijini Nairobi wamelalamika kunguni wanawatafuna.

Wasafiri wengine wanaolalamikia kero hiyo ni wale wa masafa marefu ambao wameomba Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA), kuondoa magari ambayo yanasambaza kunguni.

Ikumbukwe kuwa maelfu ya mabasi hubeba abiria pamoja na mizigo kutoka mitaani hadi katikati mwa jiji la Nairobi kila siku, hilo likiashiria uwezekano wa kunguni kuvamia matatu.

Taifa Leo Dijitali imetangamana na baadhi ya wasafiri kutoka Rongai, Kaunti ya Kajiado ambao wanaungama kuwa inawalazimu kuvumilia tu kwa sababu hawana njia nyingine ya kufika jijini.

Shughuli za usafiri katika steji. Wasafiri wengi wamelalamika kutokana na ongezeko la kunguni kwenye magari ya usafiri wa umma. PICHA|RICHARD MAOSI

“Tumekuwa tukiimba mtandaoni hata kwenye vyombo vya habari lakini wapi, ifahamike kuwa matatu nyingi hazipuliziwi dawa wala kusafishwa hivyo basi kutengeneza mtandao wa mazingira mazuri ya kunguni kuzaana,” anasema Brian Okumu mwanafunzi wa Chuo kimoja eneo la Rongai.

Anaomba NTSA kwa ushirikiano na Wizara ya Uchukuzi kulazimisha wamiliki wa matatu kupulizia magari yao dawa kuua wadudu hao hatari, angalau mara moja kwa wiki, lau sivyo wachukuliwe hatua kisheria.

Taifa Leo Dijitali pia imetambua baadhi ya viti vya magari huwa vimechanika na kunguni huwa wamekithiri kwenye magari ambayo viti vimeundwa kwa vitambaa au magodoro.

Aidha anasema wamiliki wa magari ya umma wanapaswa kuonyesha vyeti vya magari yao kupuliziwa dawa.

Kulingana na Okumu, wenye magari wanafaa sio tu kufanyiwa mafunzo ya usalama barabarani, bali pia jinsi ya kuendesha biashara katika mazingira safi.

Kulingana na data, asilimia 58 ya wakazi Nairobi hutumia magari ya Uchukuzi wa Umma kuwafikisha sehemu zao za kazi.

Utafiti huu ulifanywa na Kenya Institute for Public Policy Research Analysis.

 

  • Tags

You can share this post!

Sherehe ya ‘Sapanaa’ kutawaza viongozi katika jamii ya...

Ruto apata ‘nyaunyo’ kwa jina Felix Koskei...

T L