• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Spurs wakomoa Watford na kuweka hai matumaini ya kuingia nne-bora EPL

Spurs wakomoa Watford na kuweka hai matumaini ya kuingia nne-bora EPL

Na MASHIRIKA

BEKI Davinson Sanchez alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili na kuwavunia waajiri wake Tottenham Hotspur ushindi wa 1-0 dhidi ya Watford katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi uwanjani Vicarage Road.

Bao la Sanchez lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na mshambuliaji Son Heung-min aliyepoteza nafasi nyingi za wazi licha ya kusalia uso kwa macho na kipa Daniel Bachmann mara kadhaa. Spurs kwa sasa wanakamata nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 33, mbili pekee nyuma ya Arsenal wanaofunga mduara wa nne-bora.

Hata hivyo, Spurs ambao sasa hawajapoteza mchuano wowote wa EPL chini ya kocha Antonio Conte, bado wana mechi mbili zaidi za kusakata ili kufikia idadi ya michuano 20 ambayo imepigwa na Arsenal.

Josh King angalifungia Watford bao mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila juhudi zake zikazimwa na kipa Hugo Lloris.

Mechi hiyo ilikuwa ya sita mfululizo kwa Watford kupoteza ligini na sasa wanashikilia nafasi ya 17 kwa alama 13, tatu pekee kuliko Norwich City wanaovuta mkia. Burnley ambao wamecheza mechi 16, mbili kuliko 18 ambazo zimetandazwa na Watford, wanakamata nafasi ya 18 kwa alama 11 sawa na nambari 19 Newcastle United.

Conte aliweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa Spurs kuepuka kichapo katika mechi saba za kwanza za EPL baada ya masogora wake wakuambulia sare dhidi ya Southampton mnamo Disemba 28, 2021. Ushindi wa Spurs dhidi ya Watford uliweka hai matumaini ya kikosi cha Conte kukamilisha kampeni za EPL muhula huu ndani ya mduara wa nne-bora na hivyo kufuzu kwa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2022-23.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ruto atoboa siri yake na Mudavadi

FATAKI: Wanawake walio mamlakani wasiogope kupambana na...

T L