• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Ruto kutoza ushuru wa juu kwa samaki kutoka China kuwapa wafugaji samaki na wavuvi wa Nyanza sababu ya kutabasamu

Ruto kutoza ushuru wa juu kwa samaki kutoka China kuwapa wafugaji samaki na wavuvi wa Nyanza sababu ya kutabasamu

NA LABAAN SHABAAN

AKIENDELEZA ziara yake katika eneo la Nyanza, Rais William Ruto amezidi kutoa ahadi za maendeleo akiweka zingatio kwa uimarishaji wa shughuli za uvuvi na ufugaji samaki.

Jumamosi, Oktoba 7, 2023, ilikuwa zamu ya Kaunti ya Homa Bay kumpokea rais aliyeahidi kufanikisha maendeleo maeneo yote nchini pasi na kujali kama wakazi walimpigia kura au la.

Rais alianza mpango wa maendeleo Nyanza kwa kuzindua Kituo cha Huduma ya Samaki na Mafunzo cha Kabonyo, Kaunti ya Kisumu.

“Ninaanza mradi wa Kabonyo wa karibu Sh1 bilioni kurejesha samaki katika Ziwa Victoria ili wavuvi wetu wakienda pale wapate samaki watuletee,” alisema Dkt Ruto alipohutubia wakazi wa Mfangano, Homa Bay.

Alikuwa ameandamana na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.

Kadhalika, kiongozi wa nchi alisema moja ya njia za kuimarisha sekta ya uvuvi wa eneo la Nyanza ni kuweka ushuru kudhibiti uagizaji samaki kutoka mataifa mengine kama vile China.

 “Nimesema wale samaki wanaletwa kutoka nje ya Kenya, hao samaki wanatoka China tumesema tunaweka ushuru kama njia ya kudhibiti. Samaki tutapata hapa kwa vijana wetu na wavuvi kutoka hapa nyumbani,” aliongeza.

Takwimu za Idara ya Uvuvi zinaonyesha thamani ya samaki wanaogizwa kutoka Uchina ilikuwa kwa asilimia 25 mwaka wa 2021 na kufika viwango vya juu sana vya Sh2 bilioni mwaka wa 2022.

Rais alisema haya huku akitarajiwa kwenda China kwa mashauri ya mikopo ambapo Kenya inafuata mkopo wa Sh150 bilioni kuendeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika kituo cha redio cha Inooro Oktoba 6, 2023, Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema bosi wake ataenda Uchina kuomba fedha hizo kukamilisha miradi iliyokwama.

“Katika mashauriano hayo, rais ataomba serikali ya Uchina itathmini masharti ya huduma ya mikopo ambayo haijalipwa na pia kutupa fedha zaidi ya kukamilisha miradi ya barabara iliyokwama,” alisema Bw Gachagua.

Kiongozi wa taifa alizidi kuahidi wakazi wa Nyanza kuwa ataimarisha miundomsingi ya uvuvi kwa kukita vyumba baridi kuhifadhi samaki, viwanda vya kusindika na vituo vya kutua kwa vyombo vya majini vyenye gharama ya zaidi ya Sh1 bilioni.

 “Tunataka kuhakikisha kwamba sehemu zote za Ziwa Victoria zina miundomsingi itakayosaidia wavuvi wawe na vifaa vya kusaidia uchumi wa kaunti za Nyanza,” Rais alieleza.

  • Tags

You can share this post!

Raia wa Haiti ughaibuni waandamana wakiita Kenya kikaragosi...

Mwanamuziki Kambua Mathu asimulia pandashuka za maisha...

T L