• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Serikali kuchunguza kiwango cha fedha inachopoteza kila siku kupitia ufisadi

Serikali kuchunguza kiwango cha fedha inachopoteza kila siku kupitia ufisadi

NA STEVE OTIENO

SERIKALI ya Kenya Kwanza inalenga kufanya uchunguzi kubaini ikiwa madai kwamba Kenya inapoteza Sh2 bilioni kila siku kama ilivyoelezwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta 2021 ni ya kweli.

Haya yalisemwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Bw Felix Koskei, wakati wa mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Mashirika ya Kiraia jijini Nairobi.

Bw Koskei alisema tayari kuna mtu ambaye amejitolea kufadhili uandaaji wa ripoti hiyo.

“Mimi siwezi kubaini ikiwa madai hayo ni ya kweli au ya uongo. Hata hivyo, kuna mtu aliye tayari kufadhili uchunguzi ili kubaini kiwango halisi cha fedha tunazopoteza kwa siku na ripoti itatolewa,” alisema Bw Koskei.

Mkuu huyo wa Utumishi wa Umma alisema serikali haitakubali ufisadi wowote na kuwaonya watumishi wa umma dhidi ya kujihusisha na vitendo vya ufisadi. “Watumishi wote wa umma watakaopatikana na hatia ya kujihusisha na ufisadi watachukuliwa hatua. Kunaweza kuwa na watu wenye mashaka tunapopambana na ufisadi, lakini nawahakikishieni kuwa, tukiongozwa na Rais, tuko makini katika kazi hii. Matokeo yataonekana hivi karibuni.”

Mashirika ya kiraia, yakiwemo Haki Afrika, County Governance Watch, Siasa Place, International Budget Partnership, Mzalendo Trust, Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) yalihimizwa kuendelea kuhamasisha umma kuhusu madhara ya ufisadi.

“Kama serikali, tutashirikiana nanyi (mashirika ya kiraia) na taasisi nyingine ili kuondoa uozo ulioletwa na ufisadi katika nchi yetu. Tunahitaji kila mmoja kuwa sehemu ya vita hivi,” akaongeza Bw Koskei.

Ili kukabiliana na ufisadi ifaavyo, Bw Koskei alisema ni lazima kwanza Wakenya waelewe kuwa maovu hayo, yanayojumuisha hongo, ulaghai, unyang’anyi kati ya mengine hayakubaliki katika jamii.

  • Tags

You can share this post!

Jombi ashindwa kula siku tatu baada ya kugundua aliyepanga...

Subirini kidogo tu, hali itakuwa shwari, Ruto asihi Wakenya

T L