• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
Subirini kidogo tu, hali itakuwa shwari, Ruto asihi Wakenya

Subirini kidogo tu, hali itakuwa shwari, Ruto asihi Wakenya

ERIC MATARA na CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto jana alisisitiza kuwa mpango wa kuwekeza bajeti katika kilimo umeanza kuzaa matunda, na kwamba hivi karibuni bei ya vyakula itapungua.

Alisema wakati wa sherehe za Mashujaa mjini Kericho kwamba kupunguza bei ya mbolea kutoka Sh7,000 hadi Sh3,500 kunatarajiwa kuwezesha wakulima kuvuna magunia 61 milioni ya mahindi mwaka huu. Kulingana na rais, hili litakuwa ongezeko la karibu asilimia 50 ya mavuno ikilinganishwa na mwaka jana.

“Ndio sababu juhudi zetu katika kupunguza gharama ya maisha zitafanikiwa. Tumejikita zaidi katika kuongeza uzalishaji wa kilimo na kupanua kiwango cha ardhi kinachotumika kuzalisha chakula,” akasema.

Mbolea ya bei nafuu ndio mpango pekee kwa kuwapa afueni wananchi, ambao serikali ya Kenya Kwanza iliudumisha kutoka kwa serikali iliyotangulia.

Wakati huo huo, Rais alitetea miswada minne kuhusu Afya kwa Wote (UHC) aliyotia saini Alhamisi akisema inalenga kufanikisha mpango wa serikali yake ya Wakenya wanapata huduma za afya kwa gharama nafuu.

Hii ni licha ya kwamba mkazi wa Nairobi amewasilisha kesi mahakamani kupinga Sheria mpya ya Bima ya Hazina ya Afya ya Kijamii (SHIF), akisema kuwa sheria hiyo haijafafanua hazina hiyo itafaidi Wakenya wote au wale watakaokuwa na uwezo wa kuichangia pekee.

Lakini akihutubu alipoongoza sherehe ya 60 ya Mashujaa Dei katika mjini Kericho kiongozi wa taifa alisema chini ya mpango huo, serikali itagharamia matibabu ya afya kwa Wakenya ambao hawatakuwa na uwezo wa kuchangia bima hiyo mpya.

Dkt Ruto alisema kuwa SHIF itachukua nafasi ya Bima ya sasa ya Hazina ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) ambayo alisema imefeli kwa kuzongozwa na ufisadi pamoja na usimamizi mbaya.

“Chini mpango huu mpya kila Mkenya atapokea huduma za matibabu bila kujali ikiwa yeye ni tajiri ama masikini. Wakenya wenye mapato watalipia hazina mpya ya bima ya afya ya kijamii kwa misingi ya kiwango cha mapato yao. Yule hasla au mama mboga atalipa kiwango cha chini na matajiri kama mimi William Ruto ninayepokea mishahara wa shilingi milioni moja kwenda juu pia watalipa kiwango chao,” Rais akasema alipolihutubia taifa katika uwanja wa Michezo wa Kericho Green.

Miswada mingine ambayo Rais Ruto alitoa saini Alhamisi ni pamoja na; Mswada wa Afya ya Kimsingi, 2023, Mswada wa Afya Kidijitali, 2023 na Mswada kuhusu Ufadhili wa Mpango wa Uimarishaji Vifaa vya Matibabu, 2023.

“Sheria hizo zitaleta mabadiliko makubwa katika mpango wa utoaji huduma za matibabu nchini; zitaokoa maisha, kuziwezesha jamii kuendelea na shughuli za uzalishaji mali na kujenga taifa thabiti na yenye watu wenye afya nzuri,” Dkt Ruto akaeleza.

Kiongozi wa taifa alisema kuwa hazina tatu zimebuniwa kutokana na sheria hizo tatu, ambazo ni; Hazina ya Afya ya Kimsingi, Hazina ya Afya ya Kijamii na Hazina ya kushughulikia Dharura na magonjwa sugu.

“Hazina hii ya Dharura na Magonjwa sugu itasaidia wakati ambapo fedha za Mkenya katika hazina ya afya ya kijamii imemalizika. Hii ina maana kuwa waathiri wa ajali na wale wanaogua magonja sugu kama kansa bado watapokea matibabu katika hospitali zozote za serikali bila changamoto zozote,” Rais Ruto akasema.

“Hii inaafiki hitaji la Kipengele cha 43 (2) cha Katiba, kwamba hakuna Mkenya atanyimwa matibabu ya dharura wakati wowote kwa misingi yoyote ile,” akaongeza.

Wakati huo huo, wahudumu wa afya ya kijamii (CHP) jana walikula kiapo cha utendakazi kabla ya Rais Ruto kuzindua rasmi mpango wa UHC.
Wakiongozwa na Waziri wa Afya wa Afya Susan Nakhumicha wahudumu hao, kutoka sehemu mbalimbali nchini ,waliapa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu mkubwa na moyo wa kujitolea.

Rais Ruto alitangaza kuwa kwa mara ya kwanza chini ya utawala wa Kenya Kwanza wahudumu hao wa afya ya kijamii watakuwa wakilipwa marupurupu ya kuwawezesha kujikimu kimaisha.

“Jumla ya wahudumu 100,000 ambao wataendesha hudumu kote nchini pia wamepewa vifaa maalum vya kazi. Aidha, serikali kuu pamoja na zile za kaunti zimewanunua simu 110, 000 za kisasa ambazo watazitumia kunakili data za wagonjwa na kuzituma kidijitali katika makao ya Wizara ya Afya,” akasema.

Rais Ruto alisema kuwa serikali yake tayari imetenga Sh3 bilioni zitakazotumiwa kulipa wahudumu wa CHP marupurupu.

“Tumeelewana na Serikali za Kaunti kwamba zitatoa kiasi cha pesa sawa na hicho ili kufanisha mpango huo,” akaongeza.

Lakini katika kesi aliyoiwasilisha katika Mahakama Kuu Bw Dominic Oreo anataka mpango huu ufutiliwe mbali akisema Sheria ya Hazina ya Afya ya Kijamii (SHIF) haifafanua waziwazi ikiwa Wakenya wote watafaidi.

Aidha, Bw Oreo anataka mahakama hiyo iamuru kwamba wafanyakazi wote wa NHIF wahamishwe katika hazina hiyo mpya bila kuhitajika kuwasilisha maombi mapya ya kazi.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kuchunguza kiwango cha fedha inachopoteza kila...

Serikali inawahadaa Wakenya kuhusu uwepo wa mbolea ya bei...

T L