• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Shilingi ya Kenya ilidorora enzi za Uhuru lakini ikatiwa nakshi ionekane ina nguvu, Gavana wa CBK adai

Shilingi ya Kenya ilidorora enzi za Uhuru lakini ikatiwa nakshi ionekane ina nguvu, Gavana wa CBK adai

LABAAN SHABAAN Na CHARLES WASONGA

SHILINGI ya Kenya imedorora dhidi ya sarafu za kigeni hadi viwango vya chini zaidi katika historia.

Sasa, Dola moja  inabadilishwa kwa zaidi ya Sh150 kwa mujibu wa viwango vilivyochapishwa na Banki Kuu ya Kenya (CBK).

Lakini, utawala wa sasa unaonekana kunawa mikono kuwa haujafanya dhambi na hawafai kulaumiwa kwa shilingi kuzidi kuwa duni katika kipindi cha mwaka mmoja.

Mnamo Septemba 13, 2023, Rais William Ruto alipochukua hatamu za uongozi kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta, Dola moja ya Amerika ilikuwa sawa na Sh120.

Gavana wa CBK Kamau Thugge amesema Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia zina mtazamo tofuati kuhusu ‘kudorora’ kwa shilingi.

Akitegemea ripoti za mashirika haya, Dkt Thugge aliambia Bunge la Kitaifa Jumanne Oktoba 24, 2023 kuwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola imeongezwa thamani visivyo.

“Ninadhani kwa miaka kadhaa sasa, tumekuwa na kiwango cha ubadilishaji cha thamani kupita kiasi. Ukirejelea miaka sita iliyopita, kulikuwa na mjadala mkali kama shilingi imepewa thamani ya juu sana. Wakati huo, Taasisi za Bretton Woods zilihisi thamani ya shilingi ilizidishwa kupita kiasi kati ya asilimia 20 na 25,” Dkt Thugge alisema.

“Kuongezwa huku kwa thamani kulikuwa bayana mwaka jana. Mfumuko wa bei ulikiuka  viwango ambavyo vimewahi kushuhudiwa kwa miongo. Amerika iliongeza viwango vya riba kwa asilimia 5,” aliongeza.

Hebu tutathmini hali ilikuwa vipi miaka kadhaa iliyopita wakati Dola ilikuwa Sh120.

Mnamo Agosti, 26, 2020, Waziri wa Hazina ya Kitaifa wakati huo Ukur Yatani aliambia Bunge la Kitaifa kuwa ilibidi serikali itafute mbinu ya kudhibiti mfumuko wa bei na kudorora kwa shilingi.

“Tulitarajia kuwa kufikia sasa thamani ya shilingi itakuwa katika kiwango cha Sh120 kwa Dola kwa sababu ya janga la Corona. Lakini tumefaulu kudhibiti hali kwa kutumia akiba ya fedha za kigeni kutoka kwa Hazina ya Kimataifa ya Fedha(IMF), Banki ya Ustawi wa Afrika (ADP) na Banki ya Dunia,” alisema Balozi Yatani.

Dkt Thugge anasema CBK imeweka mikakati kadhaa ili kuimarisha shilingi ya Kenya.

Mojawapo ni kutathmini vipindi vya kubadilishana sarafu (tenor swaps) na mifumo mingine ya kufadhili sarafu humu nchini.

“Vipindi vya kubadilishana sarafu ambapo banki zisizojulikana zinahusika ni zaidi ya miezi sita,” alisema Dkt Thugge akieleza vipindi hivi havina ukomo miongoni mwa banki za humu nchini na za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kadhalika, Gavana wa CBK alisema anatarajia kiwango kikubwa cha pesa kumiminika bankini mwao kutoka IFM, Banki ya Dunia na taasisi za fedha za kikanda ili zisaidie kuimarisha shilingi ya Kenya.

Kwa mujibu wa mawasilisho yake bungeni, kikosi cha maafisa wa IMF kitazuru Kenya juma lijalo.

Hapa, hazina ya kitaifa ina matumaini ya kupata angalau $400 milioni (Sh60 bilioni).

Zaidi ya hayo, Dkt Thugge alisema Kenya inatarajia $530 kutoka IMF hivi karibuni na $750 (Sh562.5 bilioni) kutoka Banki ya Dunia kufikia Machi 2024.

CBK itatumia mkutano wa IMF kujaribu kuwarai waongeze viwango vya pesa wanavyopanga kutoa kama mkopo.

Dkt Thugge aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Fedha Jumanne kwamba data kutoka Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa kiwango cha ubadilishanaji cha shilingi ya Kenya kiliongezwa kwa kati ya asilimia 20 na asilimia 25 wakati huo wa utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Dkt Thugge alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani kuelezea sababu zinazochangia kudorora kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni, haswa dola ya Amerika.

“Kwa hivyo, wakati mmoja tulikuwa na hifadhi ya kudumu miezi 5.5 lakini sasa kipindi hicho ni miezi 3.7 ya kutumia kununua bidhaa kutoka nje. Hifadhi hii bado inatosha kushughulikia hali yoyote ya dharura. Hata hivyo, viwango vya hifadhi za pesa za kigeni vimekuwa vikishuka kutokana na kupanda kwa thamani ya sarafu za kigeni,” Dkt Thugge akawaambia wabunge wanachama wa kamati hiyo ya Fedha.

Kufikia Jumatano, Oktoba 25, 2023, dola moja ya Amerika ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh150 za Kenya.

Hii ni tofauti na hali ilivyokuwa Oktoba 2022 ambapo dola moja ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh124.

  • Tags

You can share this post!

Kansa: Mwanamke asimulia jinsi mume alivyomuacha kwa...

Mwanamke aliyejipanga kwa kununua ploti Mavoko na Njiru...

T L