• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Mwanamke aliyejipanga kwa kununua ploti Mavoko na Njiru sasa huenda akapoteza kila kitu

Mwanamke aliyejipanga kwa kununua ploti Mavoko na Njiru sasa huenda akapoteza kila kitu

NA NYABOGA KIAGE

KWA muda wa wiki moja, Bi Christine Lornah amepoteza milki aliyokuwa amewekeza kwa miaka 21 kutokana na ubomoaji uliofanyika katika eneo la Mavoko, Athi River, Machakos.

Lakini japo “radi haipigi mahali pamoja mara mbili”, uamuzi wa juzi wa korti kuwa maskwota wanaoishi eneo la Njiru, Embakasi Mashariki wanafaa kuhama kufikia Desemba 31 au wahamishwe kwa nguvu, ni kinyume cha imani hiyo ya radi.

Taifa Leo ilimpata Bi Lornah nyumbani kwake, Njiru, alikoeleza kwa masikitiko jinsi alivyoshangaa kubaini kuwa mashamba kadhaa aliyokuwa nayo katika eneo la Mavoko hayakuwa halali, bali yalikuwa mali ya Kampuni ya Kutengeneza Saruji ya East African Portland Cement (EAPCC).

Maelfu ya wakazi waliokuwa wamekaa na hata kujenga nyumba eneo hilo walitazama majengo yao yakibomolewa kwa uamuzi wa mahakama mjini Machakos, kwamba ardhi hiyo inamilikiwa na EAPCC.

Katika pigo jingine, mama huyo wa watoto wanne ni miongoni mwa maskwota 1,000 ambao Jumatatu waliagizwa kuondoka katika shamba hilo linalomilikiwa na bwanyenye Gerrishon Kirima.

“Niko katika nyumba hii japo siamini kwamba katika siku chache zijazo, sitakuwa hapa kwa sababu nililaghaiwa kununua ploti katika shamba lililomilikiwa na mtu mwingine. Ninaomba watupe nafasi, tufanye makubaliano kuhusu vile tutawalipa, nao waturuhusu kuendelea kukaa hapa,” akasema Bi Lornah.

Bi Lornah alisema alinunua shamba hilo katika eneo la Njiru mnamo 2015 na akaanza kujenga mara moja, kwani alikuwa amechoka kukaa katika nyumba ya kukodisha.

Alinunua shamba hilo kutoka kwa mnunuzi mwingine aliyehitaji pesa kwa dharura kulipia deni la hospitali.

Kulingana naye, aliponunua shamba hilo, wauzaji walimshauri aanze kujenga mara moja kwani huenda mtu mwingine akalinyakua na kuanza kujenga hapo.

“Wakati huo, nilikuwa nikiishi mtaa wa Kariobangi katika nyumba ya vyumba viwili. Wazo la kuishi katika nyumba yangu mwenyewe lilikuwa likinisukuma sana. Sikusita. Nilianza kujenga mara moja.”

Ombi lake tu ni kwamba, watu walio katika shamba hilo wanafaa kuruhusiwa kufanya kikao na familia ya marehemu Kirima na kufanya uamuzi wa pamoja, badala ya kuruhusu tofauti zao kuendelea kuongezeka, hali ambayo baadaye itawaletea hasara.

Bi Lornah alisema alichukua mikopo kujenga nyumba yake, hivyo itakuwa hasara kubwa kwake kuipoteza kwa sababu ya kuhadaiwa na mtu.

Anasema aliingia katika nyumba hiyo hata kabla ya ujenzi wake kukamilika na amekuwa akinunua vifaa tofauti vya ujenzi akiendelea kukaa ndani yake.

“Nilikuwa tu nimemaliza kujenga jikoni na bafu. Nyumba hii haikuwa na madirisha mnayoyaona. Badala yake, nilikuwa nimeweka karatasi hapo,” akasema.

Wiki mbili zilizopita, Bi Lornah pia alihamishwa kwa nguvu na kupoteza mashamba manne katika eneo la Mavoko, yaliyomgharimu jumla ya Sh1 milioni. 

  • Tags

You can share this post!

Shilingi ya Kenya ilidorora enzi za Uhuru lakini ikatiwa...

Ole Sapit alaani hatua ya wazungu kulazimishia Waafrika...

T L