• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Shinikizo maspika wa mabunge yote wawe na digrii

Shinikizo maspika wa mabunge yote wawe na digrii

NA COLLINS OMULO

SHINIKIZO za kuwataka maspika wa Bunge la Kitaifa na mabunge ya Kaunti kuwa wamefuzu kwa shahada ya digrii zimeshika kasi, huku waundasheria wakijadili mswada uliowasilishwa kwa Seneti.

Mlalamishi, Simon Lenguiya, amehoji kuwa hali ya kukosa maarifa ya kielimu na kitaaluma yanayohitajika ili mtu ateuliwe kama spika wa asasi tatu za uundaji sheria, ina athari ya moja kwa moja kwa ajenda ya sheria.

Amelisihi Bunge kurekebisha sheria ili zijumuishe masharti ya kuwa na shahada ya digrii ili mtu achaguliwe kama Spika wa bunge la kaunti, Seneti au Bunge la Kitaifa.

Kamati ya Seneti kuhusu Haki na Sheria sasa imeunga mkono mapendekezo hayo ya kuitisha shahada.

Katika ripoti iliyowasilishwa Seneti, Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Bomet, Bw Hillary Sigei, ilipendekeza sheria hizo zirekebishwe ili kuwashurutisha maspika kuwa na digrii.

Endapo mabunge yote yatakubaliana na kamati, wanaoshikilia nyadhifa hizo, watashurutishwa kuwa na digrii.

Kamati hiyo imependekeza kuwa Bunge lirekebishe Kifungu 106 (1) (a) cha Katiba kuhusu spika na manaibu wa spika ili kutenganisha masharti yanayohitajika ili mtu ateuliwe kama Spika wa Bunge na yanayohitajika kwa wabunge.

Kulingana na Katiba, matakwa yanayohitajika ili mtu achaguliwe kama Spika wa Bunge lolote lile, yanaambatana na masharti ambayo ni sharti yatimizwe ili mtu achaguliwe kama Mbunge.

Sheria inasema: “Kutakuwa na Spika kwa kila Bunge, atakayechaguliwa na Bunge hilo kuambatana na Kanuni za Bunge kutoka miongoni mwa watu waliofuzu kuchaguliwa kama wabunge lakini wasio wabunge.”

Kuhusiana na Manaibu wa maspika, sheria inasema kuwa mgombea kutoka kila Bunge atachaguliwa na Bunge husika kuambatana na kanuni, kutoka miongoni mwa wanachama wa Bunge hilo.

Hata hivyo, sheria imekimya kuhusu suala la kufuzu kielimu au kitaaluma.

Isitoshe, Kamati inataka Bunge kurekebisha Kipengee 21(1) cha Sheria ya Uchaguzi (Nambari. 24 ya 2011), ili kutenganisha matakwa yanayohitajika ili mtu awe Spika wa Bunge la Kaunti na yanayohitajika kwa madiwani.

Sheria inasema: “Spika wa Bunge la Kaunti atachaguliwa na kila bunge la kaunti kuambatana na Kanuni za Bunge la Kaunti kutoka miongoni mwa watu waliofuzu kuchaguliwa kama madiwani lakini si madiwani.”

Ili kusuluhisha udhaifu huo kwenye sheria, ripoti hiyo imeirai Bunge kuunda sheria kuhusu masharti yanayohitajika ili mtu awe Spika wa bunge la kaunti, Seneti au Bunge la Kitaifa.

Kwa sasa, Katiba na Sheria kuhusu uchaguzi haisemi chochote kuhusu masharti ya kielimu yanayohitajika kwa anayeshikilia afisi ya spika wa Bunge la Kaunti, Seneti au Bunge la Kitaifa.

“Wadhifa wa Spika wa Bunge la Kaunti, Seneti au Bunge la Kitaifa ni wajibu muhimu katika mfumo wa kidemokrasia ya nchi ambao ni sharti uzingatiwe kwa makini unavyotekelezwa, ikiwemo masharti yanayohitajika ili mtu afuzu kutwikwa wadhifa huo,” ilisema ripoti.

 

  • Tags

You can share this post!

Nyota wa West Ham Jarrod Bowen machozi tu mpenziwe Dani...

Makahaba wapandisha bei wakilalamikia polisi na Mungiki...

T L