• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Sina uwezo wa kupunguza bei ya mafuta – Ruto

Sina uwezo wa kupunguza bei ya mafuta – Ruto

NA WYCLIFFE NYABERI

RAIS William Ruto amesema hana uwezo wowote wa kupunguza bei ya mafuta ya petroli na bidhaa zake kwa kuwa bei hiyo huamuliwa na wauzaji.

Kiongozi wa taifa badala yake amesema bei ambazo anaweza kushughulikia kuzizusha ni zile zinazoambatana na gharama ya maisha, akisisitiza kuwa ameweka juhudi kubadilisha hali.

Akihutubu Jumamosi alipozuru Kaunti ya Kisii, Dkt Ruto alisema ana mpango kabambe utakaowawezesha Wakenya kupata afueni na wataanza kuona matunda ya kazi yake hivi karibuni.

“Nilipokuwa nikitafuta kazi hii nilikuwa na mpango. Tuambiane ukweli. Sina uwezo wa kushusha bei ya mafuta kwa kuwa hiyo inaamuliwa na wanaoyauza. Yale nitakayofanya ili kushusha gharama ya maisha ni kupunguza bei ya mbolea ili wakulima wazalishe chakula kwa wingi. Nitazidi kuajiri walimu, kujenga nyumba za gharama nafuu na vituo vya kidijitali ili vijana wetu wapate nafasi na ajira za kujimudu,” Dkt Ruto akasema alipohudhuria hafla ya kuchangisha pesa katika Kanisa Katoliki la Dayosisi ya Kisii katika eneo la Mosocho.

Mbali na kudondoa yale ambayo ameyafanya kwa mwaka mmoja afisini, aliwarai Wakenya waunge mkono utawala wake huku akitetea safari zake za mara kwa mara nje ya nchi, akisema zina manufaa mengi kwa taifa hili.

“Siwezi kukaa Sugoi tu wakati ninafaa kuipigia Kenya debe. Kuna makelele mengi yanayopigwa kuhusu safari zangu lakini acheni niwaambie kwamba safari hizo ni za manufaa tele. Kila mtu sasa anataka kuja hapa Kenya na ndiyo sababu mliona tukisema watu hawafai kuwa na visa ili kuzuru,” Dkt Ruto alisema.

Rais William Ruto akiwa katika Kaunti ya Kisii mnamo Desemba 16, 2023. Amekaribishwa na Gavana wa Kisii Simba Arati. PICHA | RUTH MBULA

Kwenye ziara hiyo, rais aliandamana na naibu wake Rigathi Gachagua, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, magavana Simba Arati (Kisii), Amos Nyaribo (Nyamira), wabunge kadha na viongozi wengine.

Bw Rigathi aliwaeleza watu wa jamii ya Abagusii kukumbatia mpango wa serikali wa kujenga nyumba za bei nafuu kwani  nyumba hizo zitawafaa.

Naibu Rais ambaye ni mbunge wa zamani wa Mathira, pia aliwaomba wakazi wa Gusii kuunga mkono utawala wa Kenya Kwanza huku akisema watu wa eneo hilo hawafai kuachwa kwenye kijibaridi cha kutokuwa ndani ya serikali.

“Watu wa Gusii jipangeni nyuma ya huyu rais. Yeye ndiye mwenye kisu cha kugawa nyama na hivyo msipotelee msituni,” Bw Gachagua alirai.

Mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda na Naibu Gavana wa Kisii Dkt Robert Monda, walipata wakati mgumu kuhutubia waumini hao kanisani.

Soma Pia: Mbunge Zaheer Jhanda azomewa kwa kudai Rais Ruto hana uwezo kupunguza bei ya mafuta

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro afariji familia za watu 23 waliofariki...

Maombi yakikataa kufanya kazi ‘faster’...

T L