• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
UDA yajitenga na pendekezo la Cherargei kuhusu kuongezwa kwa muhula wa Rais kuhudumu

UDA yajitenga na pendekezo la Cherargei kuhusu kuongezwa kwa muhula wa Rais kuhudumu

NA CHARLES WASONGA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) chake Rais William Ruto, kimejitenga na pendekezo la Seneta wa Nandi Samson Cherargei kwamba muhula wa kuhudumu wa rais unafaa kuongezwa kutoka miaka mitano hadi miaka saba.

Kwenye taarifa katika vyombo vya habari Jumatatu, Septemba 25, 2023, Katibu Mkuu wa chama hicho Cleophas Malala alisema pendekezo hilo haliwakilishi msimamo wa UDA au wa Rais Ruto kama kiongozi wake.

Bw Malala alisema Rais Ruto aliapa kuzingatia na kulinda Katiba ya sasa inayosema kuwa Rais ataruhusiwa tu kuhudumu kwa mihula miwili ya miaka mitano kila moja.

“Chama cha UDA kinaheshimu pendekezo la kibinafsi la Seneta huyo. Lakini kuhusiana na suala hilo la muhula wa kuhudumu kwa rais, mapendekezo hayo hayawakilishi msimamo wa chama cha UDA na/au kiongozi wake Rais William Ruto,” akasema.

Bw Malala alisema kuwa wakati huu, chama hicho tawala kinajishughulisha na haja ya kutimiza ahadi ambazo viongozi wake walitoa kwa Wakenya wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2023.

Alisema kuwa hivi karibuni chama hicho kitatoa ripoti ya utendakazi wake kwa Wakenya ili waipige msasa kwa misingi ya ratiba ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao.

“Kwa hivyo, kwa heshima, mjadala kuhusu muhula wa kuhudumu kwa Rais hauna maana yoyote na hatuhusiki nayo,” Bw Malala akasema.

Wiki jana, Seneta Cherargei ambaye ni mwandani na mtetezi sugu wa Rais Ruto aliwasilisha memoranda kwa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo akipendekeza kila muhula wa kuhudumu kwa Rais uongezwe kutoka miaka mitano hadi saba.

Hii ina maana kuwa ikiwa pendekezo hilo litakubalika, Rais Ruto atakuwa huru kuhudumu kwa miaka mingine 14 baada ya kukamilisha muhula wake wa sasa wa miaka mitano.

Kulingana na Bw Cherargei, muda wa miaka 10 anaoruhusiwa Rais kuhudumu wakati huu ni “mfupi” sana kwake kutekeleza ahadi zote alizoorodhesha kwenye manifesto yake.

“Muda mfupi kati ya uchaguzi mmoja na mwingine ndio ya ushindani mkali ambayo nyakati zingine husababisha machafuko. Ama kwa hakika muhula mmoja wa miaka mitano, hautoshi kwa Rais kuwahudumia Wakenya kikamilifu,” akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Historia Kipchoge akitawala Berlin Marathon mara ya 5  

Ujenzi wa barabara Lamu kukabiliana na Al-Shabaab  

T L