• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Ujenzi wa barabara Lamu kukabiliana na Al-Shabaab  

Ujenzi wa barabara Lamu kukabiliana na Al-Shabaab  

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI imezindua ujenzi wa barabara za usalama Kaunti ya Lamu kusaidia kukabiliana na kero ya Al-Shabaab.

Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, Rhoda Onyancha, alizindua ujenzi huo eneo la Juhudi, Lamu Magharibi mwishoni mwa juma lililopita.

Mwezi uliopita, serikali kupitia kwa Mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani) na Aden Duale (Ulinzi), walifichua mpango wa kujenga barabara sita za usalama Lamu, hasa eneo la Msitu wa Boni, ambalo limeshuhudia changamoto ya utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.

Barabara hizo sita za usalama ni ile ya kilomita 21 ya Witu-Pandanguo, barabara ya kilomita 40 ya Mkokoni-Kiunga, Bodhei-Kiunga, Pangani-Bodhei-Kiunga, Kiangwe-Basuba na Witu-Sendemke-Katsaka Kairu.

Akiongoza uzinduzi wa barabara hizo, Bi Onyancha alisema zitasaidia maafisa wa usalama kutekeleza majukumu yao kudumisha usalama na kukabiliana na adui kwa wepesi zaidi.

Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, Rhoda Onyancha akihutubu wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara Lamu kusaidia kukabiliana na majangili wa Al-Shabaab. PICHA|KALUME KAZUNGU

Aliwahakikishia wanakandarasi wanaojenga barabara hizo usalama, akisema maafisa wa kutosha wa usalama watatumwa maeneo husika wakati ujenzi ukiendelea.

Mshirikishi huyo wa usalama aidha aliwashauri wananchi kushirikiana vilivyo na walinda usalama na kutoa ripoti zitakazosaidia kukabiliana na kuwaangamiza magaidi wa Al-Shabaab na wahalifu wengine eneo hilo.

“Mara nyingi walinda usalama wetu wametatizika wakati magaidi wanapovamia maeneo haya. Utapata barabara ni tatizo, hivyo kukosa kumkabili adui vilivyo. Utapata hata unafuata nyayo na kisha zinapotea hivyo. Ndiyo maana leo tuko hapa kuzindua ujenzi wa barabara zitakazosaidia maafisa wetu kupambana vilivyo na wahalifu,” akasema Bi Onyancha.

Aliwasihi wananchi kuwa macho na kutoa ripoti zozote kuhusu tukio au mtu wanayemshuku kuwa kero kwa usalama.

Viongozi walioandamana na Bi Onyancha wakati wa uzinduzi huo ni; Naibu Gavana wa Lamu, Raphael Munyua, Mbunge wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama na Seneta wa Lamu, Joseph Githuku, ambao waliahidi ushirikiano wao na serikali kuu katika kuhakikisha usalama wa wananchi wao na mali inalindwa.

“Usalama udhibitiwe vijijini kwa manufaa ya wananchi wetu na maendeleo,” akasema Bw Githuku.

  • Tags

You can share this post!

UDA yajitenga na pendekezo la Cherargei kuhusu kuongezwa...

Haiti: Kenya ikae chonjo isiingie mtego wa Amerika

T L