• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Historia Kipchoge akitawala Berlin Marathon mara ya 5   

Historia Kipchoge akitawala Berlin Marathon mara ya 5  

NA GEOFFREY ANENE

ELIUD Kipchoge sasa ametupia jicho kupata medali ya tatu ya mbio za kilomita 42 kwenye Olimpiki 2024 baada ya kuibuka mfalme wa Berlin Marathon kwa mara ya tano nchini Ujerumani, mnamo Jumapili, Septemba 24, 2023.

Kipchoge amepongezwa na wapenzi wa riadha wakiwemo Rais William Ruto, Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga na washikilizi wa rekodi za dunia Faith Kipyegon na David Rudisha kwa kuandikisha historia hiyo.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya saa 2:01:09, Kipchoge alikamilisha umbali huo kwa 2:02:42 akifuatiwa na Mkenya Vincent Kipkemoi (2:03:13) na Muethiopia Tadese Takele (2:03:24).

Alikuwa bega kwa bega na Derseh Kindie kabla ya kusalia mbele pekee baada ya kilomita 32 wakati Muethiopia huyo alijiondoa.

“Ingawa sikupata rekodi ya dunia nilivyotarajia, kila mbio kwangu ni kama funzo. Nataka kushinda medali kwenye Olimpiki mwaka ujao (2024),” alifichua Kipchoge.

Mkenya Sheila Chepkirui aliridhika na nafasi ya pili katika kitengo cha kinadada kwa muda 2:17:49 baada ya Muethiopia Tigst Assefa kuhifadhi taji kwa rekodi mpya ya dunia ya 2:11:52.

Assefa alivunja rekodi ya Mkenya Brigid Kosgei ya 2:14:04 iliyowekwa kwenye Chicago Marathon mwaka 2019.

Rais Ruto alimvulia kofia Kipchoge akisema, “Matokeo ya kihistoria baada ya kushinda Berlin Marathon kwa mara ya tano. Pongezi kwa nyota wetu asiye na kifani Eliud Kipchoge kwa kuonyesha ustadi mkubwa Berlin Marathon2023.”

Bw Odinga aliongeza kuwa Kipchoge alidhihirisha umahiri kwa kuhifadhi taji lake.

“Hongera! Hakuna binadamu asiyeweza kufika mbali,” akasema kiongozi huyo wa upinzani Kenya.

Mshikilizi wa rekodi za dunia mbio za mita 1,500, maili moja na 5, 000m Faith Kipyegon, ambaye atashiriki makala ya kwanza ya Riadha za Dunia za Barabarani jijini Riga nchini Latvia mnamo Oktoba 1, hakuachwa nyuma kummiminia sifa Kipchoge.

“Hongera mshauri wangu Eliud Kipchoge sio tu kwa kushinda Berlin Marathon 2023, bali pia kwa kuandikisha historia ya kuwa mwanamume wa kwanza kutawala Berlin Marathon mara tano,” alisema bingwa huyo wa dunia na Olimpiki mbio za 1,500m atakayeingia kambini ugani Kasarani, Jumatatu, Septemba 25, 2023.

Mbio hizo zilipeperushwa mbashara na runinga ya NTV, huku mashabiki mjini Eldoret pia wakifurahia kuzitazama katika hoteli ya Eka kupitia ushirikiano wa Ubalozi wa Ujerumani nchini Kenya na hoteli hiyo.

Nafasi tatu za kwanza zilituzwa Sh7.2 milioni, Sh3.7m na Sh1.8m, mtawalia.

Matokeo (Septemba 24, 2023)

Wanaume – Eliud Kipchoge (Kenya) 2:02:42, Vincent Kipkemoi (Kenya) 2:03:13, Tadese Takele (Ethiopia) 2:03:24, Ronald Korir (Kenya) 2:04:22, Haftu Teklu (Ethiopia) 2:04:42, Andualem Shiferaw (Ethiopia) 2:04:44, Amos Kipruto (Kenya) 2:04:49, Philemon Kiplimo (Kenya) 2:04:56, Amanal Petros (Ujerumani) 2:04:58, Bonface Kiplimo (Kenya) 2:05:05.

Wanawake – Tigst Assefa (Ethiopia) 2:11:53, Sheila Chepkirui (Kenya) 2:17:49, Magdalena Shauri (Tanzania) 2:18:41, Zeineba Yimer (Ethiopia) 2:19:07, Senbere Teferi (Ethiopia) 2:19:21.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wa Azimio Magharibi wawashutumu Kuria na Ndii

UDA yajitenga na pendekezo la Cherargei kuhusu kuongezwa...

T L