• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Uingereza yalipa familia 2 fidia ya ng’ombe 98 kwa mali iliyoibwa

Uingereza yalipa familia 2 fidia ya ng’ombe 98 kwa mali iliyoibwa

NA ROBERT KIPLAGAT

ILIKUWA furaha kuu kwa familia mbili kutoka ukoo wa Loita wa jamii ya Maasai eneobunge la Narok Kusini zilizowapokea ng’ombe 98 kutoka Chuo Kikuu cha Oxford kama ridhaa kwa vifaa vya kale vya kitamaduni “vilivyoibwa”.

Vito hivyo vimekuwa vikihifadhiwa katika makavazi ya Pitt Rivers kwa miaka 138 na vinaaminika kusafirishwa hadi Uingereza kinyume cha sheria nyakati za ukoloni.

Ufichuzi huo ulifanywa na msomi mmoja wa Narok Bw Samuel Sankiriaki, ambaye alikuwa ametembelea makavazi hayo.

Akiongea wakati wa hafla ya utakaso kwa jina ‘Inkirro’ katika eneo la Loita mwishoni mwa wiki, Bw Sankiriaki alisema alishangaa sana kuona vifaa hivyo vya kale.

“Nilikuwa katika makavazi hayo mwaka wa 2017 na nilishangaa kugundua baadhi ya vifaa vya kale vya jamii ya Maasai. Maelezo kwenye vifaa hivyo yaliashiria kuwa vilitoka Kenya. Niliuliza jinsi ambavyo vilifika hapo,” akasema Bw Sankiriaki.

Alisema vifaa hivyo viliwahi kutumika kwa manufaa ya kibiashara ilhali wenyewe wamezama kwenye lindi la umaskini. Vifaa hivyo vinajumuisha Enkononkoi (mikufu ya wanaume) inayovaliwa na wazee, Emonyorit (mikufu ya wanawake), Isikra (kofia za wasichana waliokeketwa) na Isutia (mkufu maalum).

Alisema kuwa kulikuwa na vifaa 100 vya kale vya Kimaasai lakini vitano vilikuwa “nyeti” sana.

Maafisa wa Chuo Kikuu cha Oxford wakiongozwa na Profesa Laura Van Broekhoven, ambaye ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya makavazi, walikubali kuwa taasisi hiyo ina vifaa hivyo kutoka jamii ya Maasai ambavyo vililetwa hapo enzi za ukoloni lakini vitano vilipelekewa hapo kimakosa.

“Bw Sankiriaki alipozuru makavazi yetu na akaona vifaa hivyo, alikasirika. Alihoji mbona vifaa hivyo vilihifadhiwa hapo na hapo ndipo tuligundua kuwa vina umuhimu mkubwa kwa jamii hiyo,” akasema Profesa Broekhoven.

Alisema kuwa idadi kubwa ya vifaa hivyo ilikuwa zawadi.

Profesa Broekhoven alisema kuwa vifaa hivyo viligunduliwa kutoka eneo la Loita na familia zilizotambuliwa na nabii wa jamii hiyo Laibon Ole Mokombo.

Vifaa hivyo viligunduliwa kuwa mali ya familia za Sululu na Mpaima na kila moja ya familia hizo ilipokea ng’ombe 49 wa kike kama ishara ya amani na maridhiano.

  • Tags

You can share this post!

CASs wapokonywa minofu mdomoni

AMINI USIAMINI: Kuna buibui wanaoweza kumla ndege

T L