• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Ulimi wa Ruto wamweka hali mbaya Mlimani

Ulimi wa Ruto wamweka hali mbaya Mlimani

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto yuko hatarini kujikwaa kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya, kufuatia semi zake ambazo zimefasiriwa kama kuwakosea heshima viongozi katika eneo hilo.

Katika siku za hivi karibuni, Dkt Ruto amekuwa akitumia semi kali dhidi ya viongozi wa ukanda huo, ambao wanaonekana kutomuunga mkono na badala yake kuegemea upande wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Baadhi ya viongozi ambao wamejipata matatani ni magavana James Nyoro (Kiambu) na Kiraitu Murungi (Meru).

Akihutubu Jumapili katika eneobunge la Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu, Dkt Ruto alimshambulia vikali Bw Nyoro, akisema “anapaswa kufahamu kwamba wafuasi wa Jubilee wana akili kujiamulia mwelekeo wa kisiasa wanaotaka”.

Dkt Nyoro ni miongoni mwa magavana katika eneo la Mlima Kenya wanaounga mkono handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Gavana huyo pia ni miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa wakivumisha azma ya Bw Odinga kuwania urais mwaka ujao.

“Tuliungana pamoja 2012 na kubuni serikali ambayo haina ukabila wala chuki ya aina yoyote ile. Tulijenga barabara, reli na kuwawekea Wakenya stima. Tuliungana tena na kubuni serikali nyingine 2017. Niwaulizeni, kuna mtu anaweza kutuambia tumekosa mtu wa kutuongoza hadi tuletewe Raila aje kutuongoza? Si hayo ni madharau makubwa? Ambieni akina (Gavana) Nyoro tuna akili,” akasema Dkt Ruto.

Akihutubu Jumatatu katika Kaunti ya Meru, Dkt Ruto alimkabili Bw Kiraitu kwa njia iyo hiyo, akisema hapaswi kuishinikiza jamii ya Ameru kuhusu kiongozi watakayemuunga mkono kuwania urais.

“Gavana Kiraitu anapaswa kuwaacha watu kufanya maamuzi kuhusu kiongozi wanayemtaka kuwania urais. Anapaswa kukoma kuwashinikiza wenyeji kumuunga mkono Raila Odinga. Anataka kuwaletea mtu anayejulikana kwa ghasia na kuvunja vyama. Anapaswa (Kiraitu) kuambiwa kuwa hilo halitafanyika,” akasema.

Kutokana na kauli hizo, baadhi ya viongozi wamejitokeza kukashifu matamshi yake, huku wengine wakisema kuna hatari kiongozi huyo akaanza kupoteza uungwaji mkono aliokuwa nao katika eneo hilo.

Mbunge Kanini Keega (Kieni) anasema ni mwiko miongoni mwa jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA) kwa mwanasiasa yeyote kuwakosea heshima viongozi, wazee na tamaduni za jamii hizo kwa jumla.

“Hata ikiwa Dkt Ruto analenga kuwarai wenyeji wa Mlimani, ni lazima awahesimu viongozi waliochaguliwa. Mbona hatumwoni akiwaingilia viongozi katika maeneo mengine nchini?” akashangaa mbunge huyo.

Wadadisi wa siasa wanasema ingawa ni kawaida kwa wanasiasa ‘kuchimbiana’ nyakati za kampeni, mipaka inapaswa kuwepo.

“Ni wazi wanasiasa huwa wanafanya kila wawezalo kuwashambulia na kuwapaka tope washindani wao. Huenda mbinu wanazotumia zikawanyima umaarufu,” asema Bw Wahome Gikonyo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Ikizingatiwa eneo hilo ni kati ya yale Dkt Ruto analenga kumuunga mwaka ujao, wadadisi wanasema anapaswa kutahadhari

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Kenya ina kila sababu kujali hali ya majirani

Joho ageuka mteja ‘Baba’ akizuru Pwani

T L