• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Joho ageuka mteja ‘Baba’ akizuru Pwani

Joho ageuka mteja ‘Baba’ akizuru Pwani

Na WAANDISHI WETU

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, kwa mara nyingine alikosekana katika ziara ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga, maeneo ya Pwani.

Bw Joho ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa ODM, kwa muda mrefu alikuwa mstari wa mbele kumwandalia Bw Odinga njia zake kila anapozuru Pwani.

Hata hivyo, katika miezi ya hivi karibuni, imekuwa nadra kwake kuonyesha ukakamavu katika siasa za Pwani.

Hii ni mara yake ya pili mwaka huu kukosa ziara kubwa ya Bw Odinga Pwani, baada ya nyingine iliyofanyika Machi.

Bw Joho alikuwa katika msafara wa Bw Odinga alipozuru Dubai mapema mwezi huu Novemba, lakini baadaye akaelekea Norway kwa mikutano ya kutafuta ushirikiano wa kibiashara kwa niaba ya Kaunti ya Mombasa, na duru zikafichua alikuwa Dubai kufikia Jumanne.

“Gavana alichaguliwa na watu wa Mombasa ili kuwatumikia, na analipa hilo jukumu kipaumbele. Mahali aliko ng’ambo anatia sahihi makubaliano muhimu sana yatakayofaidi Mombasa,” afisa katika serikali ya Bw Joho aliyeomba asitajwe jina kwa kukosa mamlaka ya kuzungumzia ziara zake, aliambia Taifa Leo.

Kukosekana kwa Bw Joho kunatokea wakati ambapo ODM inakumbwa na tishio la kupoteza umaarufu katika ngome zake kuu za Pwani, hasa Kaunti za Kilifi, Kwale na Mombasa ambako Bw Odinga alizoa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Hii ni kutokana na wimbi linalovumishwa na Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kikiongozwa na Naibu Rais William Ruto, na Pamoja African Alliance kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi.

Mnamo Jumatatu, UDA ilifanikiwa kumnasa Bw Mohammed Amir ambaye ni kaka mkubwa wa Gavana Joho. Bw Amir amepanga kuwania useneta kupitia chama hicho.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Amir hata hivyo alisema uamuzi wake kuhama ODM ni wa kibinafsi.

“Nina maono ambayo yanatofautiana na yale ya familia yangu. Azimio langu ni kubadilisha maisha ya wananchi. Lakini msimamo wangu haumaanishi tunatofautiana kifamilia. Hatuchanganyi mambo ya familia na siasa. Ninafanya kile ninachoamini ni sawa. Nahisi tunahitaji mabadiliko,” akasema.

Kaimu Katibu wa Kaunti ya Mombasa, Bw Joab Tumbo, alisema hatua hiyo ya Bw Amir haifai ifasiriwe kumaanisha ODM inatikiswa Mombasa.

“Kakake amejiunga na mrengo unaoshindana na ODM, na gavana ni naibu kiongozi wa ODM. Kwa hivyo ni wazi kuwa uaminifu wa gavana ni kwa ODM,” akasema.

Katika hotuba zake za awali, Bw Joho alisema aliamua kuelekeza macho na nguvu zake kwa siasa za kitaifa.

Wakati ambapo gavana huyo anayetumikia kipindi chake cha pili hukosekana katika hafla za Bw Odinga Pwani, jukumu hilo lilikuwa likiachiwa Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir.

Hata hivyo, kufuatia ajali iliyosababisha vifo vya wafanyakazi wanne wa afisi yake Jumamosi, Bw Nassir alisitisha shughuli zake za kisiasa kwa muda.

Baadhi ya wandani wa Gavana Joho pamoja na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, ndio walioonekana wakijaza pengo hilo.

Bw Nassir na Bw Shahbal wanatarajia kushindania tikiti ya ODM kuwania ugavana Mombasa mwaka 2022.

Viongozi waliohutubu katika mikutano ya hadhara ya ODM waliambia wakazi wa Pwani wasitekwe na wimbi jipya la kisiasa ukanda huo.

“Kama kule Mlima Kenya watu wameanza kumkubali Raila Amolo Odinga na nyinyi mmekuwa mkimpigia kura wakati wote katika chaguzi zilizopita, nawaomba hakikisheni kura zake zijae, na huko kwingine itakuwa ni kujazia na atakuwa ameingia ikulu,” akasema Mbunge wa Ndaragwa, Bw Jeremiah Kioni.

Licha ya kujitenga na siasa za Pwani, Bw Joho aliandamana na Bw Odinga kwa mikutano ya kisiasa Kaunti ya Meru mwezi uliopita.

Katika mwezi huo huo, aliongoza msafara wa kuhamasisha wananchi wajisajili kupiga kura Nairobi.

Katika kaunti yake ya Mombasa, shughuli za kuongoza msafara wa kuhamasisha watu wajisajili kupiga kura uliachiwa Bw Nassir, Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, mwenzake wa Jomvu Badi Twalib na Seneta Mohamed Faki.

You can share this post!

Ulimi wa Ruto wamweka hali mbaya Mlimani

Washukiwa 3 walivyohepa gereza Kamiti

T L