• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Visa vya moto, migomo vyaongezeka katika shule za Ganze mtihani wa KCSE ukichungulia

Visa vya moto, migomo vyaongezeka katika shule za Ganze mtihani wa KCSE ukichungulia

NA MAUREEN ONGALA

MWILI wa mwanafunzi wa Kidato cha Pili ambaye aliaga dunia wakati bweni liliteketea katika Shule ya Upili ya Godoma mnamo Jumatatu asubuhi, unahifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Kaunti ya Kilifi.

Kamishna wa Kilifi Bw Josephat Biwott amethibitisha kwamba mwanafunzi aliangamia kwenye mkasa huo ambao umejiri wakati visa vya moto na migomo vimeongezeka katika shule za eneobunge la Ganze katika kipindi cha mwezi mmoja.

Akizungumza na wanahabari, Bw Biwott alisema kuwa kamati ya usalama ya kaunti ya Kilifi imeanzisha uchunguzi wa kutaka kujua sababu ya visa vya ghafla vya wanafunzi kuchoma shule.

“Tunataka kujua kwa nini ghafla tu wanafunzi katika eneobunge la Ganze wameanza kugoma na kuchoma shule,” akasema.

Aidha aliwaonya walimu wakuu na wazazi kuwa ni hatia kwa wanafunzi kuchoma shule.

Mbunge wa Ganze Bw Kenneth Kazungu amesikitika huku akitaka viongozi katika eneo hilo kuungana kukabili changamoto ya migomo ya kila mara katika shule za eneobunge hilo.

“Tunajitahidi kila mara kuinua hadhi ya kaunti ndogo ya Ganze lakini kila tunapofanya hivyo, kitu kinatokea na kuturudisha nyuma ,” amesema Bw Kazungu.

Mnamo Jumapili usiku, wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Mwangea waligoma.

Shule nyingine ambako visa vya aina hiyo vimeshuhudiwa ni shule ya wavulana ya Ganze, na za wasichana za Ganze, Bandari na Kachororoni.

Siku ya kutathmini utayarifu wa watahiniwa wa mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023) ni Oktoba 19, 2023, huku mtihani wenyewe ukitarajiwa kuanza Oktoba 23, 2023.

Mnamo Septemba 2023 mbunge huyo alikosoa Wizara ya Elimu kwa kuzembea katika kutatua changamoto zinazokumba shule ambazo zimekuwa chanzo cha migomo.

Mbunge wa eneo hilo aliwataka maafisa katika wizara huyo wang’atuke ikiwa wameshindwa kazi ya kukagua shule na kudhibiti visa vya moto na migomo kila mara.

  • Tags

You can share this post!

Afanyiwa kiini macho akapapasa nyani akidhani ni kimada wake

Ndoa ya mitara inatambulika kisheria, Karen Nyamu ajitetea...

T L