• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Wafuasi wa Azimio wasema mambo bado

Wafuasi wa Azimio wasema mambo bado

Na GEORGE ODIWUOR

WABUNGE wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM)Raila Odinga wamejitetea dhidi ya madai kwamba walishindwa kutetea Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa.

Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti Alhamisi kwamba Naibu wa Rais Dkt William Ruto “alishinda raudi ya kwanza ya Mswada huo” wakati wa majadiliano ya mswada huo unaopendekeza kubuniwa kwa sheria ya kutambua miungano ya kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 2022.

Wakati wa majadiliano ya mswada huo yaliyowasilishwa na kiongozi wa wengi bungeni Bw Amos Kimunya mnamo Jumatano bunge liliahirisha vikao vyake hadi Januari 2022 baada ya mbunge mmoja mwandani wa Dkt Ruto kuwasilisha mapendekezo 17 katika mswada huo wa marekebisho.

Ilibidi Bunge liahirishe vikao vyake kuwezesha kamati ya Sheria na Haki kutathmini na kupiga darubini mapendekezo ya marekebisho yaliyowasilishwa na mbunge mwandani wa naibu wa Rais kabla ya kujadiliwa na bunge lote.Kuahirishwa kwa vikao vya bunge ilikuwa kinyume na matarajio ya Bw Odinga na wandani wake waliotazamia kupitisha miswada hiyo Jumatano kuwezesha kubuniwa kwa muungano wa Azimio la Umoja utakaomteua kinara huyo wa ODM kuwa mwaniaji wake wa wadhifa wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti Bw Ruto aliibuka na ushindi katika raudi ya kwanza ya mjadala huo bungeni.Lakini wabunge wa mrengo wa ODM walikanusha madai hayo huku wakisema “ni wao walioibuka na ushindi kwa mujibu wa idadi ya wabunge waliohudhuria kikao cha Jumatano.”

Mwakilishi wa kina mama kaunti ya Homa Bay Bi Gladys Wanga, Mbunge wa Kasipul Bw Ong’ondo Were na mwenzake kutoka Karachuonyo Bw Adipo Okuome walisisitiza walishinda mjadala huo. Wanasiasa hao walisema hayo Alhamisi walipozugumza katika mkutano uliofanyika katika wadi iliyoko Karachuonyo kaunti ya Homa Bay.

Bw Odinga alikuwa amehudhuria mkutano huo.Bi Wanga alisema ilidhihirika wazi kwamba Naibu wa Rais Dkt Ruto hana uungwaji mkono bungeni.’Walikuwa wanajigamba wako na idadi kubwa ya wabunge. Tuliwaashiria walete wabunge wao. Hatimaye walikuwa na wabunge 40,”alisema Bi Wanga.

Mbunge huyo alisema kiongozi hiyo wa ODM hapasi kutambuliwa kama “mradi wa serikali akisema Bw Odinga anaungwa mkono na wakenya wengi.”’Wakenya wanamfahamu Raila Odinaga ni nani. Amepigania nchi hii sana.Hii ndio maana yuko na umaarufu,’alisema Bi Wanga.

Bw Were alieleza matumaini yake kwamba Mswada hiyo itapitishwa mwaka ujao.Alisema wandani wa Bw Odinga wameagizwa waupitishe mswada huo.’Kupitia mwongozo wa kiongozi wetu, tuko na uhakika mswada huu utapitishwa,’ alisema Bw Were huku akiwataka Wakenya wadumishe amani.

Bw Okuome alikiri wabunge wa ODM walikumbwa na wakati mgumu bungeni lakini hawakufa moyo.Alisema kuwa Dkt Ruto hakushinda lakini alimlaumu Naibu wa Spika Bw Moses Cheboi aliyesema aliahirisha kikao cha bunge kwa pupa.Bw Odinga hakuguzia kuhusu suala la mswada huo ulioko bungeni.

You can share this post!

JUMA NAMLOLA: Krismasi iwe mwalimu kuhusu kuwajali wengine...

WANDERI KAMAU: Serikali isirejeshe enzi za giza na kuua...

T L