• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
WANDERI KAMAU: Serikali isirejeshe enzi za giza na kuua demokrasia

WANDERI KAMAU: Serikali isirejeshe enzi za giza na kuua demokrasia

Na WANDERI KAMAU

KATI ya mwaka 1964 na 1970, Kenya ilishuhudia karibu marekebisho 20 ya kikatiba.

Ingawa baadhi ya marekebisho hayo yalilenga kuigeuza Katiba ili kuwiana na mfumo mpya wa kiutawala, mengi yaliendeshwa na serikali kutimiza malengo yake.Miongoni mwa malengo hayo yalikuwa ni kumpa nguvu Rais kumtimua chamani au kumwadhibu yeyote aliyeonekana kuipinga serikali au kwenda kinyume na matakwa yake.

Mageuzi hayo bila shaka ndiyo yalikuwa chanzo cha kutimuliwa kwa baadhi ya wanasiasa maarufu kutoka KANU, kwani ndicho kilikuwa chama pekee cha kisiasa nchini wakati huo.Hilo ni baada ya viongozi wa chama cha KADU kama marehemu Daniel Moi na Ronald Ngala kukivunja na kujiunga na KANU mnamo 1960.

Mageuzi hayo yalimpa nguvu nyingi rais kiasi kwamba hangesita kumchukulia hatua mtu yeyote aliyeonekana kumkosea heshima au kuonyesha msimamo tofauti na chama.Mabadiliko hayo yalimgeuza rais kuwa kama ‘mungu’ mdogo, kwani alitumia mamlaka yake kuwashawishi wabunge kupitisha jambo lolote lililoijenga Kanu na serikali kwa jumla.

Hii ni bila kujali jinsi Wakenya wengine walivyoyapokea au kuyakumbatia mageuzi hayo.Mtindo huo uliigeuza Kenya kuwa taifa la kidikteta, licha ya kuwa na mwanzo mzuri sana miaka michache baada ya uhuru.Kiini cha urejeleo huu ni juhudi ambazo tumeona zikiendeshwa na wanasiasa kubuni vyama vya kisiasa karibu kila kuchao kwa kisingizio cha “kuwakabili” washindani wao kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kufikia sasa, ni wazi kuwa kuna zaidi ya vyama 100 vya kisiasa nchini.Kwa tathmini ya kina, vingi vimebuniwa mwaka huu, wawaniaji wengi wakihofia huenda wakakosa nafasi kwenye shughuli za mchujo zitakazoendeshwa na vyama vikubwa vya kisiasa.Kama hilo halitoshi, Bunge la Kitaifa linalenga kubadilisha Sheria ya Vyama vya Kisiasa ili kutoa nafasi kwa miungano ya kisiasa kugeuzwa kuwa vyama.

Maswali yanayoibuka ni: Mbona harakati hizi zinafanywa wakati uchaguzi mkuu unapokaribia? Kulikuwa na haja wabunge kuagizwa kurejea bungeni kupitisha mageuzi hayo? Yatamfaa Mkenya kwa njia ipi?Kimsingi, mazingira ya kisiasa tunayoshuhudia nchini yanafanana na ilivyokuwa katika miaka ya sitini, sabini na themanini, wakati wabunge walikuwa wakiagizwa kupitisha mageuzi fulani ya kikatiba kwa malengo fiche.

Ijapokuwa Bunge ni tawi kuu la serikali linalopaswa kuendesha shughuli zake kwa njia huru, ni wazi limegeuzwa kuwa kinyago na serikali ya sasa.Hilo ni sawa na kurejesha Kenya katika enzi ya giza. Ni wazi serikali inatumia uwezo wake kushinikiza mageuzi ya kikatiba kwa manufaa ya viongozi wachache bila kujali athari yatakayokuwa nayo kwa vizazi vijavyo.Huu ni usaliti wa demokrasia!

[email protected]

You can share this post!

Wafuasi wa Azimio wasema mambo bado

Sababu za Ruto kupinga vikali mswada wa vyama

T L