• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Wakazi wakumbuka mazuri Base Titanium ikijiandaa kufunga shughuli

Wakazi wakumbuka mazuri Base Titanium ikijiandaa kufunga shughuli

NA SIAGO CECE

WAKAZI wa Kaunti ya Kwale wamebaki vinywa wazi baada ya kampuni ya uchimbaji madini ya Base Titanium kutangaza kuwa itafunga mtambo wao mwaka 2024.

Baadhi ya wakazi waliisifu kampuni hiyo wakisema kuwa imekuwa ya manufaa kwa jamii kwa miaka ambayo imekuwa ikifanya uchimbaji, na kuondoka kwake kutakuwa pigo kubwa kwa jamii.

Kando na jamii, wafanyakazi zaidi ya 1,400 pia ni miongoni mwa wanaosikitika kutokana na tangazo hilo la kumaanisha kuwa kila mmoja wao atapoteza kazi.

“Base Titanium imenisaidia katika kuhifadhi mazingira kwa kupanda mikoko, na pia imeboresha hali ya afya. Base ikiondoka itakuwa mzigo mkubwa kwetu kwa sababu hii misaada ambayo wanafunzi wamekuwa wakipata haitakuwa na wazazi wataendelea kuishi maisha ya uchochole,” Bw Kondo Harun alisema.

Kampuni hiyo wiki jana ilitangaza kuwa hakuna madini yenye thamani ya kutosha katika maeneo yaliyofanyiwa utafiti katika kaunti hiyo, na hii italazimisha kampuni hiyo kufunga shughuli mwaka wa 2024 wakati madini yote yatakuwa yameisha.

Kulingana na meneja wa kampuni hiyo Simon Wall, wafanyikazi ambao asilimia kubwa ni wenyeji wa kaunti ya Kwale, watapokea ushauri nasaha ili kuwasaidia kimawazo wakati kampuni hiyo imeanza matayariho kabla kufunga.

“Tunaelewa kuwa hili ni swala kubwa sana hasa kwa familia ambazo zimekuwa zikitegemea wapendwa wao wanaofanya kazi hapa Base Titanium. Lakini tunawapa fursa ya kupata ushauri ili kujitayarisha kwa jambo hilo. Mimi mwenyewe nimesikitika,” Bw Wall alisema.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo imetoa ombi la kufanya utafiti katika Kaunti ya Lamu na eneo la Kuranze lililo katika mpaka wa Kwale na Taita Taveta.

Ikiwa serikali itakubali ombi hilo, kampuni hiyo itachukua zaidi ya miaka mitatu kabla kuhakikisha kuwa madini hayo yana thamani na kuanza uchimbaji upya katika maeneo hayo.

Baadhi ya wakazi walikuwa wameipongeza Base kwa miradi yao ya kijamii katika kaunti za Kwale na Mombasa ambayo ni pamoja na zahanati, kumbi za kijamii, miradi ya maji, barabara na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa shule za upili.

Miradi hiyo sasa itakamilika mwaka 2024 wakati kampuni hiyo itafunga.

Hata hivyo, swala tata limebaki kwa ardhi ambayo kampuni hiyo ilikuwa ikifanyia uchimbaji wao baada ya baadhi ya wakazi waliohamishwa hapo awali wakitaka waruhusiwe kurudi ili waishi hapo upya.

  • Tags

You can share this post!

DPP aomba korti idumishe adhabu dhidi ya Oswago

DONDOO: Barobaro akemea ‘mumama’ aliyejaribu...

T L