• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 4:55 PM
DPP aomba korti idumishe adhabu dhidi ya Oswago

DPP aomba korti idumishe adhabu dhidi ya Oswago

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga ameiomba Mahakama Kuu kudumisha adhabu ya kifungo jela dhidi ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) James Oswago kwa kuhusika katika sakata ya Sh1.3 bilioni ya uagizaji wa vifaa vya uchaguzi mkuu wa mwaka 2013.

Wakili wa serikali amemuomba Jaji Nixon Sifuna adumishe hukumu dhidi ya Oswago na aliyekuwa Naibu Katibu wa IEBC aliyehusika na Masuala ya Huduma Wilson Shollei akisema mahakama iliyowahukumu ilifuata sheria.

Oswago na Shollei walitozwa faini ya Sh7.5 milioni au watumikie adhabu ya kukaa jela miaka mine kila mmoja kwa kukiuka sharia za uagizaji wa vifaa vya uchaguzi wa Machi 4, 2013.

Oswago hata hivyo anapinga akisema adhabu hiyo ilikuwa kali sana kwa yeye ambaye alikuwa mkosaji wa kwanza.

Wakikosoa hukumu iliyotolewa na hakimu Felix Kombo, Oswago na Shollei walisema alivuka mipaka yake  kwa sababu kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia Ufisadi na Makosa ya Kiuchumi, mwenye hatia anafaa kutozwa faini ya Sh1 milioni, lakini hakimu alitoza faini ya Sh5 milioni na Sh2.5 milioni za ziada kwa mashtaka mawili.

Jaji Sifuna ameratibu uamuzi kutolewa Februari 28, 2024.

Oswago na Shollei walifungwa Desemba 2022 kwa kuidhinisha malipo ya Sh1,397,724,925.51 kwa Face Technologies Limited bila kukagua au kujali kwamba vifaa vilikubalika na vilikuwa vya teknolojia iliyohitajika kwa kurejelea mkataba.

“Mahakama imezingatia changamoto za uchaguzi lakini imebaini kwamba dosari katika uagizaji wa vifaa vya kura ziliathiri matokeo kwa namna moja au nyingine,” akasema Bw Kombo wakati huo.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wagundua waliyemsaidia kupata matibabu ni jambazi...

Wakazi wakumbuka mazuri Base Titanium ikijiandaa kufunga...

T L