• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Wakongwe kupokea pesa za Inua Jamii kupitia M-Pesa

Wakongwe kupokea pesa za Inua Jamii kupitia M-Pesa

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto ametangaza kuwa wakongwe, mayatima na walemavu wataanza kupokea malipo yao ya Sh2, 000 kila mwezi kutoka kwa serikali kupitia maduka ya M-Pesa kule vijijini.

Mpango huo unaojulikana kama Inua Jamii ulianzishwa na utawala uliopita wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na unafaidi jumla ya watu milioni 1.2 waliosajiliwa rasmi.

Kiongozi wa nchi alisema hayo Jumanne, Desemba 12, 2023 alipoongoza sherehe za 60 za Jamhuri Dei Uhuru Gardens, Nairobi

“Sasa serikali imeamua kwamba wazee, mayatima na watu wanaoishi na ulemavu ambao hupokea pesa za mahitaji yao ya kimsingi kila mwezi chini ya mpango wa Inua Jamii, hawatatembea kwa mwendo mrefu. Wataweza kupata pesa hizo vijijini mwao kupitia maduka ya M-Pesa,” Rais Ruto akaeleza.

Alisema mpango huo umewezeshwa kutokana na mkataba uliotiwa saini kati ya serikali na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom.

“Safaricom itatoa huduma hii bila malipo,” Rais Ruto akaeleza alipowahutubia Wakenya wakati wa maadhimisho ya Jamhuri Dei 2023.

Dkt Ruto alisema mayatima ndio kundi la kwanza litakaloanza kufaidi kwa mpango huo mwishoni mwa mwezi huu wa Desemba.

“Wakongwe na wale wengine wataanza kupokea pesa zao kupitia M-Pesa kuanzia mwishoni mwa Januari mwaka ujao, 2024, kwa sababu tunahitaji kufanya mambo fulani kwanza,” akaeleza.

Dkt Ruto alikariri kwamba serikali yake inaendelea kutekeleza sera ambapo makundi hayo ya watu wenye mahitaji maalum hupokea malipo yao kabla ya watumishi wengine wa serikali kulipwa mishahara yao.

 

  • Tags

You can share this post!

Murang’a yamulikwa ulimwenguni kiwango cha mazao shambani...

Majirani wanatuhepa? Viongozi marafiki wa nchi wakosa hafla...

T L