• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 10:36 AM
Majirani wanatuhepa? Viongozi marafiki wa nchi wakosa hafla muhimu na ya kihistoria, ya Kenya@60

Majirani wanatuhepa? Viongozi marafiki wa nchi wakosa hafla muhimu na ya kihistoria, ya Kenya@60

NA BENSON MATHEKA

HATUA ya viongozi wa mataifa jirani na ya kigeni kukosa kuhudhuria sherehe za Jamhuri Dei jijini Nairobi imeibua maswali kuhusu mtizamo wao kuhusu sera za serikali ya Kenya Kwanza.

Hali hii ni tofauti na Rais William Ruto ambaye amekuwa akitumia mialiko anayopata kuzuru mataifa mbali mbali jirani, Afrika na ng’ambo.
Mnamo Jumapili, serikali kupitia Katibu wa Masuala ya Ndani Dkt Raymond Omollo ilitangaza kuwa viongozi watatu wa nchi za kigeni wangehudhuria maadhimisho ya 60 ya Jamhuri Dei katika bustani ya Uhuru Gardens, Nairobi.
Japo hakutaja viongozi hao na nchi zao, ilitarajiwa kuwa angalau wangetoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo mbali na kuwa jirani, nchi hizo zimeunganika na Kenya kiuchumi na kijamii.
Hata hivyo, hakuna hata kiongozi mmoja wa nchi hizo aliyehudhuria sherehe hizo akiwemo mwenyekiti wa EAC,l Rais Salvar Kiir wa Sudan Kusini.
Rais wa Belarus Aleksandr Lukashenko aliyezuru nchini Jumatatu jioni pia hakuhudhuria sherehe hizo.
Kulingana na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), Rais Lukashenko alikutana na Rais Ruto katika ikulu ya Nairobi na alitarajiwa kuhudhuria sherehe za Jamhuri jana.
“Rais wa Belarus Aleksandr Lukashenko na mwenzake wa Ethiopia Sahle Work Zewde tayari wamewasili nchini kama wageni wa Rais William Ruto katika sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya uhuru,” KBC ilisema katika taarifa mtandaoni Hata hivyo, Ikulu haikuthibitisha iwapo alikuwa amealikwa kwa sherehe hizo na
hakufika katika bustani ya Uhuru Gardens ambapo ziliandaliwa.
Baadhi ya viongozi wa mataifa jirani waliwatuma maafisa wa ngazi za chini kuwawakilisha tofauti na Rais Ruto anayependa kuhudhuria binafsi mialiko katika nchi za kigeni.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu alimtuma rais wa Zanzibar Ali Mwinyi ambaye alisema kiongozi huyo jirani wa Kenya upande wa kusini “ hakuweza kufika kwa kuwa nchi imegubikwa na mafuriko yanayosababishwa na mvua ya El Nino kaskazini mwa nchi yetu”.
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye alialikwa kuhudhuria sherehe za jana alimtuma naibu waziri mkuu wa nchi hiyo Rebecca Kadaga huku Rais wa Burundi Jenerali Évariste Ndayishimiye akiwakilishwa na makamu wake Prosper Bazombanza.
Rais Museveni jana alikuwa akizindua sensa ya sita katika nchi yake. Marais wa nchi zingine za EAC Paul Kagame( Rwanda), Salvar Kiir( Sudan Kusini), Félix Antoine Tshisekedi (DRC) na Somalia Hassan Sheikh Mohamud hawakuhudhuria huku Ethiopia ikidumisha utamaduni wake wa kumtuma rais wake Sahle-Work Zewde kumwakilisha Waziri Mkuu Abiy Ahmed. Rais Zewde alisema amekuwa akihudhuria sherehe za Jamhuri jijini Nairobi kwa miaka minane.
Mtaalamu wa masuala ya kidiplomasia James Waki anasema si lazima viongozi wa nchi za kigeni wafike binafsi wanapoalikwa na mataifa mengine japo kufika kwao huwa kunasawiriwa kama ishara ya nia na heri njema.
“Mialiko hutumwa lakini uamuzi ni wa viongozi wanaoalikwa. Wanaweza kufika binafsi au kutuma ujumbe unaoongozwa na afisa wanayechagua. Hata hivyo kufika kwao binafsi huwa na uzito kwa kusawiri uhusiano wao na nchi inayowaalika una nguvu,” alisema.
Jana, Rais Ruto kwa mara nyingine alisisitiza kwamba, kuanzia Januari, Kenya itafungua milango yake kwa raia wa nchi za Afrika na hawatahitajika kuwa na viza kuingia nchini.

  • Tags

You can share this post!

Wakongwe kupokea pesa za Inua Jamii kupitia M-Pesa

Wazee wa jamii ya Agikuyu wamkana Maina Njenga

T L