• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Waliokuwa wamestaafu waoga na kurudi katika soko la ajira

Waliokuwa wamestaafu waoga na kurudi katika soko la ajira

NA FRANCIS MUREITHI

MAELFU ya wafanyakazi wa yaliyokuwa mabaraza ya miji na serikali za kaunti waliostaafu, wamelazimika kurudi kazini kuepuka umasikini baada ya kaunti 44 kukosa kuwasilisha malipo yao ya uzeeni.

Kuna wanachama 15,842 wa shirika la malipo ya uzeeni la wafanyakazi wa serikali za kaunti (Laptrust) ambao malipo yao hayajawasilishwa na waajiri wao.

Kwa sasa, wafanyakazi 8,843 waliostaafu hawawezi kupata pensheni yao kwa kuwa pesa za pensheni walizokatwa walipokuwa wakifanyakazi kuhifadhiwa na shirika hilo hazijawasilishwa.

Laptrust linasema linadai serikali za kaunti Sh33 bilioni ambazo linapaswa kulipa wanachama wake waliostaafu pensheni zao.

Baadhi ya wafanyakazi hao wamelazimika kutafuta kazi za kuwakimu baada ya kustaafu huku serikali za kaunti zikishikilia pesa walizowekeza kama pensheni katika shirika hilo na gharama ya maisha ikiendelea kuwatatiza.

Wastaafu hao, ambao umri wao umepita miaka 60 wanalazimika kutegemea jamaa zao na marafiki kwa chakula na gharama ya matibabu.

Ripoti ya Shirika la Taifa la Takwimu (KNBS) inaonyesha kuwa, watu 776,159 kati ya 869,338 walio na umri wa zaidi ya miaka 60 walikuwa wakifanya kazi kufikia Desemba mwaka jana ikiwa ni asilimia 82.1 ya idadi ya wazee wote nchini.

Ripoti ilisema kwamba, wengi wao wanalazimika kufanya kazi ili kupata pesa za kukidhi mahitaji ya kimsingi huku 6,881 walio na umri zaidi ya miaka 60 wakijiunga na vijana wanaohitimu vyuo vikuu kutafuta kazi.

Aidha, wafanyakazi walio na umri wa zaidi ya miaka 60 wanaamua kuajiriwa kwa kandarasi baada ya kufikisha umri wa kustaafu.

Ripoti hiyo inasema kwamba, wafanyakazi walio na umri wa zaidi ya miaka 60 wanaoajiriwa kwa kandarasi baada ya kutimiza umri wa kustaafu waliongezeka kwa asilimia 7.7 kati ya Machi na Desemba 2022.

Katika kongamano la kila mwaka la Laptrust lililofanyika Nakuru, Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema: “Zaidi ya asilimia 82 ya wazee walio na umri wa miaka 60 na zaidi wamerudi kazini kwa sababu ya kukosa au kupungua kwa pensheni.”

“Wengine karibu 6,900 wanashindana na vijana wanaohitimu vyuo vikuu kutafuta kazi. Waajiri nao wanapendelea wafanyakazi walio na ujuzi. Hii inamaanisha tunafaa kuimarisha mifumo ya kinga ya jamii tunapofanya kazi na baada ya kustaafu,” alisema Bw Gachagua na kuongeza kuwa, “Mtu anayefurahia maisha ya kustaafu hawezi kurudi kutafuta kazi.”

Bw Ezra Ngoje, mfanyakazi mstaafu alisema inahuzunisha kwamba, kaunti zinawanyima pensheni pesa ambazo wanakatwa kwa uchungu wakilenga kufurahia maisha ya uzeeni.

“Hii sio zawadi. Magavana wanafaa kulipa Sh33 bilioni wanazodaiwa na LAPTRUST,” asema.

Baadhi ya magavana ambao kaunti zao zimekwamilia pesa za wastaafu ni Johnson Sakaja (Nairobi), Abdulswamad Shariff (Mombasa), Ahmed Nadhif Jamma (Garissa), Ochillo Ayacko (Migori), Simba Arati (Kisii), Gladys Wanga (Homa Bay), Ahmed Abdullahi (Wajir), Wavinya Ndeti (Machakos), George Natembeya (Trans Nzoia) na Kawira Mwangaza wa Meru.

Ripoti ya kina ya Hazina ya Taifa inaonyesha kuwa, kaunti zinadaiwa zaidi ya Sh30 bilioni na Laptrust, Sh 2.59 bilioni na CPF huku Local Authorities Provident Fund (Lapfund) likidai serikali hizo Sh31.37 bilioni kufikia mwisho wa Januari 30, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wamwambia Ruto ushuru wa juu unaramba...

Sarakasi Gavana Mwangaza akijadiliwa katika bunge la Seneti

T L