• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Wamiliki wa baa Murang’a watumia mbinu za kimafia

Wamiliki wa baa Murang’a watumia mbinu za kimafia

NA MWANGI MUIRURI

WALEVI, watengenezaji wa pombe na wamiliki wa baa katika Kaunti ya Murang’a wanaonekana kuwazidi maarifa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Gavana Irungu Kang’ata katika vita dhidi ya ulevi kupindukia.

Naibu Rais na gavana Kang’ata walikuwa na mkakati wa kupunguza baa zilizo na leseni kutoka 2,971 hadi 1,032 hivyo basi kutema 1,939.

Lengo hilo lilikuwa liafikiwe Juni 15 lakini likaahirishwa hadi Juni 30.

Lakini kufikia sasa, baa zote na nyingine 393 zilizopatikana zikihudumu bila leseni, bado zinaendelea kuhudumu baada ya kuungana kupinga viongozi hao wawili.

Katika pingamizi hizo, baa hizo zinaendelea kuhudumu bila leseni na mbinu hiyo huenda ipate Kaunti ya Murang’a ikikosa ushuru wa takribani Sh77.6 milioni.

Msasa wa kutoa leseni za mwaka wa 2023 ulikuwa umependekeza baa hizo zipunguzwe kwa asilimia 65 hali ambayo imegeuka kuwa ngumu kutekelezwa.

Hii ni baada ya walioidhinishwa kupewa leseni kuungana na waliokuwa wanyimwe kudai ni lazima njama hiyo ibatilishwe.

Gavana akihojiwa hivi majuzi katika kituo cha Inooro TV alisema kwamba “wamiliki wa baa hizo wamewasilisha kesi mahakamani ya kupinga kufungiwa biashara zao”.

Hofu ni kwamba, kesi hii ikijikokota, huenda wahudumu hao wajipate wakiuza pombe hadi Januari ambapo leseni nyingine zitatolewa.

“Bw Gachagua na Bw Kang’ata wanafaa waelewe kwamba hakuna sheria nchini inayobagua mwekezaji kuanza au kuendeleza biashara ya pombe iliyo halali. Hatua ya kutwaa leseni ya kibiashara inafaa kuafikiwa katika hali ya dharura na iliyoidhinishwa na mahakama,” akasema Bw Simon Ngugi ambaye baa zake tatu zilikuwa zifungwe.

Hatua hiyo ya kufunga baa aidha imevutia pingamizi za Muungano wa Wamiliki wa Baa, Hoteli na wauzaji pombe.

Mwenyekiti wa muungano huo Bw Simon Njoroge alisema “shughuli zinaendelea kama kawaida kwa wanachama wetu hadi mahakama iamue”.

Alisema hatua hiyo ya Bw Gachagua na Bw Kang’ata iko na hatari ya kumaliza zaidi ya nafasi za kazi 25,000 ambazo ni za mahasla ambao serikali ya Kenya Kwanza ilitumia kuingia mamlakani.

  • Tags

You can share this post!

Tatizo la wanawake kunenepa kupita kiasi lazidi –...

AMINI USIAMINI: Wapo wadudu wanaotumia kinyesi cha ndovu,...

T L