• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Wanaharakati, maafisa wasema baadhi ya wazee Malindi wana tabia mbaya ya kulawiti na kunajisi

Wanaharakati, maafisa wasema baadhi ya wazee Malindi wana tabia mbaya ya kulawiti na kunajisi

NA ALEX KALAMA

WANAHARAKATI wa kutetea haki za kibinadamu na maafisa wa idara ya urekebishaji tabia wameingiwa na hofu wakisema watoto wadogo wako katika hatari kubwa ya kufanyiwa maovu kipindi hiki ambapo shule zinafungwa kwa likizo ndefu.

Kulingana na mshirikishi wa Shirika la Malindi GBV Network Helda Lameck, kuna haja ya wazazi kuwa karibu na watoto wao msimu huu wa likizo ili kuwaepusha na tabia mbaya na hatari ya kuvuliwa utu wao.

Akizungumza na wanahabari mjini Malindi, Bi Lameck amesema kuwa licha ya wazazi kujishughulisha na kuwatafutia wana wao chakula na mahitaji mengine, ni sharti wazazi pia wafuatilie mienendo ya watoto wao.

“Hivi sasa watoto wanafunga shule kwa miezi miwili na hofu yetu kubwa ni kwamba watoto, wasichana kwa wavulana, huenda wakakumbana na changamoto tele. Najua ni lazima sisi wazazi tutafute… tuende kazi tutafute namna ya kukidhi maisha. Lakini wakati unapotoka nyumbani hao watoto unawaacha na nani na wakifanya nini? Ni lazima sisi wazazi tujiulize maswali ya aina hiyo,” alisema Bi Lameck.

Bi Lameck alieleza kuwa visa vya unajisi na ubakaji vimeongezeka Malindi.

Aidha alisema watoto wa kiume nao wanalawitiwa katika eneo hilo, hivyo basi kuna haja ya wazazi kuwalinda watoto wao.

“Kesi nyingi ambazo tumekuwa tukizipokea hapa Malindi ni za watoto wa kiume kulawitiwa ama kubakwa na akina baba au wazee, tena watu wa karibu wa familia. Ni hali ya kusikitisha sana hata sijui tunaelekea wapi. Kwa hivyo naomba kina mama kuwa waangalifu na kujua ni nani unayemuachia mtoto wako kabla ya kutoka kuenda kazi,” alisema Bi Lameck.

Kwa upande wake, msimamizi wa gereza la Mtangani mjini Malindi Bw Vincent Atonya, amefichua kuwa baadhi ya wazee walio na umri mkubwa zaidi wamekuwa wakijihusisha na dhuluma za kijinsia kwa watoto huku akiwasihi wazee wa vijiji kuripoti visa hivyo kwa asasi husika.

“Hii hali ya kesi za unajisi na ubakaji imezidi kwa sababu gerezani wamejaa watu wa kesi za ubakaji na ni wazee wa umri wa miaka 60 hadi 70. Ukweli usemwe, watu wale wako kwa vijiji hivyo tafadhalini, jaribuni kuongea na wazee wa aina hiyo. Sababu hata mimi nashangaa umri umeenda unashindwa huyu mzee na nguvu zimeisha unatafuta nini. Si utulie na umekuwa mzee mbona ujihusishe na mambo haya ya aibu? Tafadhalini, washaurini waache hiyo tabia. Mtu asiingi jela kwa sababu ya kesi ya ubakaji,” alisema Bw Atonya.

  • Tags

You can share this post!

Handisheki ya ‘siri’ yazua hofu Mlima Kenya

Njuri Ncheke wagawanyika kuhusu juhudi za kumtimua Kawira...

T L