• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Wanasiasa wageuza mjadala kuwa mzaha

Wanasiasa wageuza mjadala kuwa mzaha

WANDERI KAMAU, BENSON MATHEKA NA MARTIN MWAURA

KAULI zinazotolewa na wanasiasa na viongozi tofauti nchini kuhusu Mazungumzo ya Maridhiano ya pande mbili yanayoendelea katika Ukumbi wa Bomas, Nairobi, zimeibua wasiwasi kuhusu iwapo kuna nia njema ya kuyafanikisha.

Ijapokuwa mazungumzo hayo baina ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja yanalenga kutafuta suluhisho kufuatia mzozo wa kisiasa tangu uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kauli za wanasiasa zinaashiria wanayachukulia kama mzaha.

Hii ni licha ya wabunge wa pande zote kuunga hoja ya kutambua mchakato huo kisheria.

Baadhi ya viongozi ambao kauli zao zinafanya mazungumzo hayo kuonekana kama mzaha ni mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais William Ruto, Spika wa Seneti Amason Kingi, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa huku Waziri wa Uchukuzi na Barabara Kipchumba Murkomen, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Watang’ula wakiwa na maoni tofauti.

Hapo jana, Bw Nyoro alisema mazungumzo hayo yanafaa kusitishwa mara moja kwani “yanawapotezea Wakenya muda”.

Akihutubu katika eneobunge lake la Kiharu, Kaunti ya Murang’a, Nyoro alisema kuwa Wakenya walishiriki kwenye uchaguzi mkuu mwaka uliopita na kumchagua kiongozi ambaye wangependa awaongoze.

“Watu ambao wametuajiri (wananchi) walizungumza kwa sauti moja mwaka uliopita na kuamua kuhusu yule atawaongoza na yule atakuwa kiongozi wa upinzani au atakuwa akiangalia utendakazi wa serikali. Kwa hivyo, bila tashwishi yoyote na kwa ukweli kamili, mimi kama Ndindi Nyoro na watu wa Murang’a, Kiharu na Kenya kwa jumla, tunaomba kwamba, kesho (leo), wakati mazungumzo hayo yataanza, ajenda ya kwanza inafaa kuwa ya kuyasimamisha,” akaeleza Bw Nyoro.

Kauli kama hiyo ilitolewa majuzi na Bw Kingi, katika Kaunti ya Kilifi, aliposema kuwa mazungumzo hayo “yanaipotezea muda serikali kutimiza na kutekeleza ajenda yake ya maendeleo”.

“Hata ikiwa Rais Ruto na Raila (kiongozi wa Azimio) watafanya mazungumzo, hilo halitapunguza gharama ya maisha. Njia pekee ya kupunguza gharama ya maisha ni kumruhusu Rais kutekeleza manifesto yake,” akasema Bw Kingi.

Bw Ichung’wa, kwa upande wake, amekuwa akisisitiza kuwa hataruhusu mazungumzo hayo kujadili suala la Handisheki, licha ya Bw Odinga kusisitiza kuwa nia yake si kubuni Handisheki na Rais Ruto.

“Nikiwa kiongozi wa ujumbe wa Kenya Kwanza, sitakubali suala lolote kuhusu handisheki lijadiliwe. Hatutakubali mazungumzo hayo kutumiwa kama njia ya kuwaruhusu baadhi ya watu kuingia kwenye serikali yetu kupitia mlango wa nyuma,” akasema Bw Ichung’wa.

Hata hivyo, ijapokuwa kimsingi viongozi hao wanafaa kuonyesha msimamo sawa, ikizingatiwa wako katika mrengo wa Kenya kwanza, wake Rais Ruto, wametofautiana vikali na wenzao, ambao wametoa kauli za kuunga mkono mazungumzo hayo.

Akihutubu katika Kaunti ya Homa Bay mapema mwezi huu, Bw Murkomen aliwalaumu vikali Bw Ichung’wa (anayeongoza ujumbe wa Kenya Kwanza) na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka (anayeongoza ujumbe wa Azimio) kwa “kuwapotezea Wakenya muda”.

Aliwalaumu kwa “kuigeuza nchi kama mateka kimakusudi” kwa kuchelewesha mazungumzo hayo kuanza.

“Makundi hayo mawili yamesema hayataki serikali ya muungano (nusu mkate). Mbona viongozi hao wawili wanaipotezea Kenya muda? Wote wameorodhesha ajenda zao. Wanafaa kuzijadili haraka iwezekanavyo,” akasema Bw Murkomen.

Akaongeza: “Ikiwa mchakato huo utakosa kupata mafanikio na hali ya mapigano kurejea nchini, wao ndio watalaumiwa.”

Mwito kama huo ulitolewa majuzi na Bw Wetang’ula, aliyeomba viongozi kutohatarisha mazungumzo hayo kwa kutoa matamshi ya chuki.

“Kama Wakenya, lazima tuzungumze na kusuluhisha masuala yanayotukabili kwa uungwana,” akasema Bw Wetang’ula, Ijumaa, alipohutubu katika eneobunge la Webuye Magharibi wakati wa hafla ya kuchangisha pesa.

Hayo yalijiri huku ikiibuka kuwa vikosi vya kiufundi vilivyobuniwa na makundi hayo mawili bado havijakubaliana kuhusu masuala tata, mazungumzo hayo yanapotarajiwa kurejelewa leo.

Hapo jana, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alibaki kimya kuhusu ikiwa vikosi hivyo vimekubaliana kuhusu masuala tata au la.

“Ni kweli tunakutana kesho saa nne asubuhi kama ilivyopangwa hapo awali. Hata ikiwa ninafahamu (vikosi vya kiufundi vimekubaliana kuhusu masuala tata), siwezi kuzungumzia suala hilo. Tungoje kesho (leo) saa nne asubuhi,” akasema jana, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

  • Tags

You can share this post!

Wezi wanaolenga maduka ya bidhaa za kula na za matumizi...

Karen Nyamu anavyotumia msanii Samidoh kuvuna umaarufu...

T L