• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Wezi wanaolenga maduka ya bidhaa za kula na za matumizi nyumbani Mwihoko, Kiambu

Wezi wanaolenga maduka ya bidhaa za kula na za matumizi nyumbani Mwihoko, Kiambu

NA NYABOGA KIAGE

JAMBAZI ambaye ni miongoni mwa genge linalohangaisha wahudumu wa maduka ya bidhaa za kula eneo la Mwihoko, Kiambu ameuawa kwa kupigwa risasi na askari.

Mhalifu huyo alikumbana na mauti usiku wa kuamkia Jumapili, Agosti 20, 2023 akiwa na wahuni wenza wawili wakitorokea Mwiki, Nairobi.

Kulingana na afisa polisi aliyeomba kubana majina yake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari, watatu hao walifuatwa kuanzia Mwihoko baada ya kutekeleza wizi.

Walitumia barabara ya Eastern Bypass kukwepa mtego wa polisi.

Walikuwa wamejihami kwa bastola, na walitumia pikipiki kutorokea usalama wao.

“Walipotakiwa kusimama na kusalimu amri, aliyekuwa na bunduki alianza kufyatulia askari risasi na hatukuwa na budi ila kukabiliana naye,” kachero huyo akaambia Taifa Leo Dijitali.

Alipigwa risasi na kufariki wakati wa kizaazaa hicho, wenzake wawili wakifanikiwa kuhepa.

“Wamekuwa wakitumia silaha hiyo kuhangaisha wamiliki na wahudumu wa maduka ya bidhaa za kula na za matumizi ya nyumbani,” afisa huyo alidokeza.

Akithibitisha kisa hicho, Mkuu wa Polisi katika Kaunti ya Nairobi, Bw Adamson Bungei alisema kuwa askari wameanza kusaka majambazi waliotoroka pamoja na washirika wenza.

“Mwili wa aliyeuawa ulipelekwa kwenye Hifadhi ya Maiti ya City,” Bw Bungei alisema.

Kabla ya mchezo wa paka na panya na askari, inasemekana walivamia maduka mawili ya kuuza bidhaa za kutumia nyumbani eneo la Mwihoko, ambapo waliiba pesa na mali yenye dhamani isiyojulikana.

Walitumia bastola kutishia watu, ili kutekeleza uhalifu na kutoroka kwa kutumia pikipiki.

Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo Dijitali, walilalamikia hali ya usalama Mwihoko kudorora.

Bi Lucy Wairimu, mwenyeji, alisema wahuni hao wanatekeleza uhalifu maduka yanapofungwa jioni.

“Inasikitisha kuona silaha ambazo zinapaswa kutulinda zinatumika kutuhangaisha na isitoshe kutuibia chakula na bidhaa za matumizi ya nyumbani,” Wairimu alishangaa.

Bw Moses Limo, mkazi mwingine, alisema wakati wa wizi huo alikuwa tayari ameshafunga kazi na aliamshwa na kamsa.

Niliogopa kutoka nje kwa hofu ya usalama wangu, Limo akasema, akisikitikia usalama kudoroa Mwihoko.

  • Tags

You can share this post!

Magavana wageuka kuwa ‘miungu’ badala kuwa watumishi

Wanasiasa wageuza mjadala kuwa mzaha

T L