• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Uhuru arusha chambo kwa Mlima Kenya wapende tena Jubilee

Uhuru arusha chambo kwa Mlima Kenya wapende tena Jubilee

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA mbunge wa Ndaragwa Bw Jeremiah Kioni amefichua kuhusu mikakati mipya ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ya kuzindua harakati za ujasusi wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya akinuia kuteka nyara mijadala ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Bw Kioni akihutubia wanahabari mnamo Jumanne, Desemba 19, 2023, katika Kaunti ya Tharaka Nithi, alisema kwamba kwa sasa mrengo wa Jubilee ndani ya Azimio la Umoja-One Kenya unalenga kuteka nyara mijadala yote ya kisiasa katika kila safu ya eneo la Mlima Kenya kwa nia ya kudhibiti mtazamo wa 2027 ili wapigakura katika ngome hiyo waungane kupinga utawala wa Rais William Ruto.

Njama, akaongeza, imesukwa kuhakikisha kwamba Rais Ruto hafai kuchaguliwa tena 2027 hivyo basi historia yake kuwa wa kwanza kuhudumu kwa awamu moja pekee.

Kwa kawaida, Katiba ya 2010 hutoa awamu mbili za miaka mitano kila moja kupitia kura ya baada ya miaka mitano.

“Tunaweka mabalozi wetu katika kila Kaunti ya Mlima Kenya ambapo katika kila kaunti eneo hili kutakuwa na washirikishi wa mijadala mashinani wasiopungua 1,000. Kutoka kila kijiji hadi makao makuu ya kaunti hali itakuwa hivyo ikizingatiwa kwamba tumekuwa tukifanya hivyo katika kila kaunti na sasa mtandao wetu uko imara,” akasema Bw Kioni.

Bw Kioni aliongeza kwamba “nia yetu sasa ni kuvamia kila jukwaa la mijadala ya kisiasa…kuanzia kwa vyombo vya habari, mazungumzo kwa baa, sokoni…kila mahali  na pia tukihusisha vijana haya wa vyuo vikuu…tukihubiri ajenda ya kuingia serikalini 2027…tukionyesha watu kwamba utawala huu sio wa manufaa yetu kamwe”.

Bw Kioni ambaye hubishania ukatibu mkuu wa chama hicho wakiwa na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Kanini Kega, alisema kwamba “tutahakikisha Bw Kenyatta anatuongoza kupenya mashinani hapa Mlima Kenya.”

“Lengo letu ni kutafuta njia ya kusambaratisha umaarufu wa United Democratic Alliance (UDA),” akasema.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, chama cha UDA ambacho huongozwa na Rais Ruto, kiliaibisha hicho cha Jubilee kikiongozwa na Bw Kenyatta kwa ushindi wa asilimia 87 dhidi ya 13 eneo la Mlima Kenya.

Bw Kioni amekuwa akisisitiza kwamba Rais Ruto na wandani wake walicheza ngware tele za kisiasa bila Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kudhibiti na hali ikaishia wizi mtupu wa kura.

Ingawa hivyo, Mahakama ya Upeo nayo kwa upande wake ilitupilia mbali kupitia majaji sita katika uamuzi wa kesi iliyowasilishwa kupinga ushindi wa Ruto.

Lakini sasa, Bw Kioni ametangaza nia ya Jubilee ya kuoga na kurejea kwa soko hilo kilichokataliwa na kuibuka na mikakati thabiti ya kuwania na kuitwaa serikali mwaka wa 2027.

“Kwanza ieleweke wazi kwamba chama cha Jubilee hakitatoka mrengo wa Azimio. Tuko ndani ya mrengo huo kufa kupona na mkubwa wetu akiwa ni Bw Kenyatta hapa Mlima Kenya na kitaifa ufuasi wetu ukisalia kwa Bw Raila Odinga,” akasema.

Hata hivyo, Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu amepuuzilia mbali njama hiyo ya Jubilee akiitaja kama ndoto mbaya ya mchana.

“Hawa ni wale ambao tuliwashinda wakiwa na serikali yote mikononi mwao. Tulishindana na wawaniaji wao waliokuwa bado mamlakani sisi tukiwa tu watu wa kawaida na tukaibuka na ushindi. Sasa ni sisi serikali na tuko mamlakani huku Bw Kenyatta wao na Bw Kioni wao wakiwa raia tu wa kawaida,” akasema.

Alimkumbusha Bw Kioni kwamba hata sasa chama cha Jubilee kina mirengo miwili na kuna uwezekano mkuu hivi karibuni mrengo huo wa Kenyatta upigwe marufuku ya kutumia jina na nembo za Jubilee.

Bw Kenyatta na mbunge maalum Bi Sabina Chege wanazozania na kung’ang’ania nafasi ya kiongozi wa chama.

“Kile hatutakubali ni siasa kuchezwa Mlima Kenya kwa nia ya kuhujumu umoja na uwiano na watu ambao wanafikiria kusambaza ukaidi na ukosefu wa matumaini ndio mbinu ya kuwarejesha mamlakani watu walioyatumia vibaya na kuishia kutupwa nje na wapigakura,” akadai Bw Nyutu.

Bw Nyutu alidai kwamba kuchapa kampeni za ukosefu wa matumaini hakutakubalika kwa kuwa ni sawa na kuzindua kanisa la kisiasa lenye misingi isiyoleta faida isipokuwa aibu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Jombi alia tangu mke kupandishwa cheo kazini, kabweteka...

Watoto 700 kusherehekea Krismasi, Mwaka Mpya jelani

T L