• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Wazee watangaza kuhubiri amani 2022

Wazee watangaza kuhubiri amani 2022

Na KNA

BARAZA la Wazee katika Kaunti ya Mombasa limejitolea kuhubiri amani na kutoa ushauri kwa wananchi na wanasiasa kuhusu umuhimu wao wa kudumisha amani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Wanachama wa baraza hilo sasa wanaitaka serikali kuu kuwapa usaidizi ili waweze kutekeleza jukumu hilo na kutatua mizozo ambayo inaweza kusababisha vita miongoni mwa wanajamii.

Katika mkutano na maafisa wa usalama Mombasa chini ya uongozi wa Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Gilbert Kitiyo, wazee hao walikubaliana kwamba watashirikiana na serikali katika juhudi za kuhakikisha amani inasambaa katika kaunti hiyo.

“Serikali inahitaji usaidizi kuhusiana na suala hili, hasa kutoka kwa wazee. Kuna mengi mwaweza kufanya na mumewahi kufanya ila hayajaandikwa. Ninaamini mwaweza kutusaidia kudumisha amani katika kaunti hii kuelekea uchaguzi mkuu ujao,” akasema Bw Kitiyo.

Naibu Mwenyekiti wa baraza hilo Askofu Joseph Maisha alisema Baraza la Wazee Mombasa lilibuniwa mnamo 2013 kuelekea uchaguzi mkuu ili kuwahudumia wakazi wa Mombasa na kuhubiri amani.

“Hili ni jukwaa ambapo wazee hujadili masuala yanayowaathiri wananchi kama vile amani, tamaduni, elimu, vijana, michezo na mengine mengi hadi ngazi za mashinani,” akasema Maisha.

Baraza hilo lilisema litashirikiana na Kamati ya Usalama, Kaunti ya Mombasa na Shirika la REINVENT kuendeleza amani katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Kitiyo aliwahimiza wazee hao kueneza jumbe za amani miongoni mwa vijana na wanasiasa.

Aliwataka kuhimiza jamii dhidi ya kuunda makundi ya vijana au magenge ya wahalifu kwa ajili ya kutumika na wanasiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Wakati kama huu wa siasa, baadhi ya wanasiasa hubuni magenge ya kutumia kuwapa ulinzi wakati wa kampeni. Wanachama wa magenge haya huwatisha na hata kuwapiga wapinzani wao,” Bw Kitiyo akasema.

Wazee hao waliapa kuanza kazi moja kwa moja hasa katika mitaa ya mabanda ambako kuna ongezeko la visa vya utovu wa usalama.

Waliahidi kushirikiana na makundi ya usalama vijijini maarufu kama Nyumba Kumi ambayo wanachama wake hutangamana na raia wa kawaida nyakati zote.

Ili kurahisisha kazi za wazee hao, Bw Kitiyo aliahidi kusaka usaidizi kutoka kwa wahisani na mashirika ya usalama yatakayowafundisha kuhusu mbinu ya kutatua mizozo na kupalilia amani katika jamii.

You can share this post!

Toyota Kenya kusambaza magari 592 kwa polisi

Kaunti za Mulembe zilitumia mabilioni kwa ziara –...

T L