• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Wito watoto wanaoishi na ulemavu watunzwe vizuri

Wito watoto wanaoishi na ulemavu watunzwe vizuri

NA LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya wazazi wenye watoto wanaoishi na ulemavu kuwapa upendo badala ya kuwatelekeza.

Mkurugenzi wa kituo cha Hope and Faith Centre for the Disabled eneo la Juja Dkt Marion Karimi amesema kuna watu wengi wanaoishi na ulemavu baadhi yao wakifurika hapa nchini kutoka nchi jirani.

“Kulingana na uchunguzi uliofanywa, imebainika kuwa wazazi wengi wenye watoto wanaishi na ulemavu hawana ujuzi kamili wa kuwalea na kwa hivyo watoto hao hupitia shida tele,” alisema Dkt Karimi.

Alisema yeye akiwa mmoja wa walio na ujuzi wa kulea watoto hao amekuwa na kibarua kigumu kwa kuwahamasisha wazazi wenye watoto hao.

Alisikitika kwa kusema ya kwamba kuna watu wengi wanaoishi na ulemavu na ambao mara nyingi huwa barabarani hasa maeneo ya  Juja, Thika na hata Ruiru.

Dkt Karimi anayehifadhi watoto wenye ulemavu wapatao 177 alisema baadhi ya watoto huwa wametelekezwa na watu wasiojulikana.

Aliyasema hayo katika kanisa la World Wide Ministry Church la Theta Ruiru ambapo alirudishia Mungu shukrani kwa kutambulika kwa kuwatunza vizuri watoto wanaoishi na ulemavu. Shahada hiyo aliipokea kutoka kwa chuo cha  Breakthrough International Bible University  kwa kazi yake ya miaka 17 akihudumia na kuwashughulikia watoto  wanaoishi na ulemavu.

Mchungaji Francis Muhia ambaye ni mumewe Dkt Karimi, alisema amekuwa mstari wa mbele kusaidia mkewe kulea watoto hao.

“Kazi hiyo imekuwa ngumu lakini Mungu amekuwa nasi muda huo wote hadi mafanikio yakapatikana,” alieleza mchungaji Muhia.

Alitoa wito kwa serikali kujenga vituo kadha vya watu wanaoishi na ulemavu na kuweka ada nafuu ya malipo ili wazazi waweze kupeleka watoto wao huko.

Alikiri kuwa wazazi wenye watoto wanaoishi na ulemavu wanapitia changamoto kubwa ya kuwalea watoto hao.

Bw Aaron Gachanja ambaye ni afisa anayelea watoto wanaoishi na ulemavu eneo la Juja alisema watoto wengi ambao huachwa peke yao na wazazi nyumbani wakati mwingi hudhulumiwa bila kutambulika.

“Kwa hivyo wazazi wawe macho wanapowaacha wana wao nyumbani,” alisema Bw Gachanja.

Alisema kila mtoto popote alipo ana uzuri wake na kwa hivyo hawapaswi kuteswa na mtu yeyote yule.
  • Tags

You can share this post!

Steven Gerrard achukua mikoba ya Al-Ettifaq

Mbunge afurahia hatua ya vijana kuacha pombe

T L