• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Afrika yaomboleza Elizabeth lakini yakumbuka udhalimu wa Uingereza dhidi ya weusi

Afrika yaomboleza Elizabeth lakini yakumbuka udhalimu wa Uingereza dhidi ya weusi

NA CECIL ODONGO

KIFO cha Malkia Elizabeth II kimetonesha vidonda vya nchi nyingi za Afrika zilizoathiriwa na ukatili wa utawala wa ukoloni wakati kiongozi huyo wa Uingereza alikuwa usukani.

Kati ya nchi ambazo zilikuwa chini ya himaya ya Uingereza ni Kenya ambayo ilipata uhuru 1963 kisha ikawa Jamuhuri mnamo 1964 malkia akiwa mamlakani.

Nchi nyingi barani Afrika ambazo zilikuwa chini ya Uingereza kama Mkoloni zililalamikia ukandamizaji, ukiukaji wa haki, unyakuzi wa ardhi zao na mauaji ya kiholela.

Mauti ya Malkia Elizabeth II yamezua kumbukumbu za madhila hayo huku baadhi ya raia wa nchi hizo wakimkashifu kuwa alipokuwa usukani, alichangia na kuunga mateso dhidi ya Waafrika.

Kiongozi wa upinzani Afrika Kusini Julius Malema alisema hakuna haja ya Afrika kuomboleza kifo cha Malkia akisema, uongozi wa Uingereza ulikuwa janga nchini humo na bara zima.

“Malkia mwenyewe alinufaika na mali iliyotwaliwa kutoka Afrika kupitia mateso na mauaji. Waafrika wengi walipelekwa Uingereza kama watumwa na kuteswa. Hakuna cha kusherehekea kutokana na mauti hii,” akasema Malema.

Wanachama wa Kundi la Mau Mau ambalo lilianza vita vya ukombozi miaka ya 50 ni kati ya wale ambao waliuawa kinyama na serikali ya ukoloni kisha ardhi zao kutwaliwa.

Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu lilikadiria kuwa Wakenya 90,000 waliuawa kinyama na wengine 160,00 kuteswa vibaya na wanajeshi wa Uingereza kabla ya Kenya kujinyakulia uhuru.

Mnamo Juni 2013, zaidi ya miaka 50 baada ya Kenya kutoka kwenye minyororo ya wazungu, aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Nje William Hague aliomba msamaha na kukubali kulipa fidia walioteswa na jamaa zao kuuawa.

Nchini Zimbabwe, kifo cha malkia hakijashangiliwa huku baadhi wakishangaza kwa kufurahia mauti yake kutokana na mateso kabla ya kupata uhuru.

“Ningekuwa na uwezo ningecheza kwenye kaburi la malkia na pia wanafamilia wengi wa ufalme wakifa. Yale waliyoyatendea Waafrika bado yapo mioyoni mwetu. Utawala wa Uingereza ulikuwa katili mno,” akasema Zoe Samudzi, mwandishi mashuhuri, Zimbabwe.

Nchini Nigeria, hali ilikuwa hiyo hiyo, wasomi na raia wakisema hawana cha kusherehekea kuhusu mauti ya Malkia Elizabeth wa Pili.

“Kama mtu anatarajia nisikitikie mauti ya Malikia, basi anaota. Ni ufalme huo ambao uliwachinja raia kinyama na kusababisha nusu ya familia yangu iishi kama wahamiaji kwenye nchi yao,” akasema Profesa Uju Anya ambaye anafundisha fasihi katika Chuo cha Carnegie Mellon.

Hata hivyo, Profesa Mathew Smith wa Chuo Kikuu cha London anasema wale ambao hawajasikitishwa na mauti ya malkia wanamlaumu kwa makosa ambayo hata si yake.

  • Tags

You can share this post!

Tafrija wanajeshi wakimuaga Uhuru

Charles III kutawazwa leo kumrithi mama yake Malkia...

T L