• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Charles III kutawazwa leo kumrithi mama yake Malkia Elizabeth II

Charles III kutawazwa leo kumrithi mama yake Malkia Elizabeth II

MASHIRIKA na WINNIE ONYANDO

MWANAMFALME Charles III anatarajiwa kutawazwa rasmi leo kumrithi Malkia Elizabeth aliyega dunia Alhamisi.

Mfalme Charles, 73, atatawazwa katika Jumba la St James’s, London, mbele ya Baraza la Upokezaji wa Mamlaka.

Baraza hilo linajumuisha wajumbe wa Baraza la Faragha – kikundi cha wabunge na vigogo wa kisiasa wa zamani na wa sasa, makamishna wakuu wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth) na Meya wa jiji la London.

Katika sherehe hiyo, kifo cha Malkia Elizabeth kitatangazwa kwa sauti na Rais wa Baraza la Faragha ambaye ni mbunge Penny Mordaunt.

Wakati wa tangazo hilo, Malkia atapongezwa kwa kazi yake.

Baada ya hapo, watu kadhaa akiwemo Waaziri Mkuu Liz Truss na Askofu Mkuu wa Canterbury ambao watatia saini kuonyesha kuwa watamuunga mkono mfalme anayeingia mamlakani.

Baada ya hapo, Mfalme atahudhuria mkutano wa pili ya Baraza la Upokezaji wa Mamlaka pamoja na Baraza la Siri.

Baada yake Mfalme atatoa tamko jipya na kulingana na mila ya mwanzoni mwa Karne ya 18 – atafanya kiapo cha kuhifadhi Kanisa la Scotland.

Baada ya hayo yote, tangazo litatolewa hadharani kuwa Charles III ndiye Mfalme mpya.

Hii itafanywa kutoka kwenye dari ya Mahakama ya Friary katika Kasri la St James’, na afisa anayejulikana kama Garter King of Arms.

Baada ya hapo, atasema “Mungu Umwokoe Mfalme”, na kwa mara ya kwanza tangu 1952, wimbo wa taifa utaimbwa huku watu wakikariri “Mungu Umwokoe Mfalme”.

Wanajeshi watafyatua mizinga katika eneo la Hyde Park, Mnara wa London na kutoka kwa meli za wananjeshi wa majini, na tangazo litasomwa kuwa Charles III ndiye Mfalme.

Bendera zitarejea kupeperushwa juu la mlingoti kwa saa 24 kuashiria kutangazwa kwa Mfalme Charles III kabla ya kurejea nusu mlingoti.

Wakati huo huo, mwili wa Malkia Elizabeth utalazwa katika Kanisa Kuu la St Giles, Edinburgh kwa siku 10 maandalizi ya mazishi yakiendelea.

Mwili wa Malkia Elizabeth utasafirishwa kwa ndege hadi London, ambapo wananchi watapata nafasi ya kumuaga.

Baada ya Mfalme Charles kutawazwa, mkewe, Camilla, Duchess wa Cornwall atakuwa Malkia mpya.

  • Tags

You can share this post!

Afrika yaomboleza Elizabeth lakini yakumbuka udhalimu wa...

Elizabeth II alipata umalkia akiwa ziara nchini Kenya

T L