• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Aliyekuwa waziri mkuu wa Japan auawa kwa risasi

Aliyekuwa waziri mkuu wa Japan auawa kwa risasi

NA AFP

KASHIHARA, JAPAN

WAZIRI Mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe jana alikufa akitibiwa hospitalini saa chache baada ya kupigwa risasi katika mkutano wa kampeni eneo la Nara, magharibi mwa nchi hiyo.

Serikali ililaani kisa hicho na kuapa kutowasamehe wahusika.

Likimnukuu afisa wa ngazi ya juu katika chama cha Abe, Liberal Democratic Party, Shirika la Kitaifa la Habari nchini Japan, NHK lilisema, “waziri mkuu wa zamani Abe alikufa hospitalini jijini Kishahara, eneo la Nara, ambako alikuwa akipokea matibabu. Alikuwa na umri wa miaka 67.”

Kifo cha kiongozi huyo pia kiliripotiwa na vyyakiwemo mashirika ya habari ya jiji kuu la Tokyo.

Kuuawa kwa mwanasiasa huyo maarufu nchini Japan kulitokea licha ya uwepo wa sheria kali dhidi ya matumizi ya bunduki nchini humo.

Aidha, aliuawa wakati wa kilele cha kampeni kuelekea uchaguzi wa bunge la seneti ambao umeratibiwa kufanyika kesho, Jumapili.

Awali, Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida alisitisha kampeni zake na kusafiri kwa helikopta hadi Tokyo ambako aliwahutubia wanahabari kwa sauti iliyojaa huzuni.

“Waziri mkuu wa zamani Shinzo Abe alipigwa risasi katika eneo la Nara na nimefahamishwa kwamba yuko katika hali mahututi,” akasema.

“Ninaomba waziri mkuu wa zamani apone haraka,” akaongeza, huku akilaani kitendo hicho cha kikatili na ambacho kimetokea msimu wa kampeni kuelekea uchaguzi.

“Hatuweza kuwaseheme waliopanga uovu huo. Ninalaani kitendo hicho kwa maneno makali mno.”

Abe alishambuliwa kwa risasi majira ya adhuhuri alipokuwa akiwahutubia wafuasi wa chama chake huku walinda usalama wakiwepo.

KIJIVU

Hata hivyo, wananchi walimkaribia kwa urahisi.Picha zilizopeperushwa na shirika la habari la NHK zilimwonyesha akiwa amesimama jukwaani. Mwanamume aliyevaa shati jeupe na long’i ya kijivu alimkaribia kutoka nyuma huku akitoa kitu fulani mfukoni na kukifyatua.

Alifyatua risasi mara mbili na kila moja ilitoa moshi. Huku watu na wanahabari wakijaribu kujiepusha na hatari, mwanamume mmoja alionekana akishambuliwa na walinda usalama na akaangushwa chini.

Baadaye alinaswa kwa tuhuma za kujaribu kutekeleza mauaji kwa kukusudia, ripoti zikasema.

Vyombo vya habari nchini Japan vilimtambua mwanamume huyo kama Tetsuya Yamagami, 41, vikinukuu duru za polisi.

Aidha, vyombo hivyo vya habari vilimwelezea kama mwanajeshi wa zamani wa kikosi cha Wanamaji nchini Japan.

Alikuwa amebeba bunduki na shirika la NHK lilisema kuwa aliwaambia polisi baada ya kukamatwa kwake kwamba alilenga kumuua Abe. Watu waliokuwepo katika eneo la tukio walielezea kushtushwa na jinsi ghasia zilivyotokea katika mkutano huo wa kisiasa.

“Mfyatuko wa kwanza uliotoa sauti ya bunduki bandia,” mwanamke mmoja aliambia NHK.

“Baada ya mlio wa pili, watu walimzingira Abe na kuanza kumpa huduma ya kwanza,” mwanamke huyo, ambaye aliomba jina lake libanwe, alieleza.

Mhudumu mmoja katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Nara aliambia AFP hivi: “Kile ambacho tunaweza kusema sasa ni kwamba uhamisho wake hadi hapa umekamilishwa”.

Hata hivyo, mhudumu huyo alidinda kufichua hali halisi ya Abe.

Vyombo kadha vya habari viliripoti kwamba waziri huyo mkuu wa zamani huenda alipigwa risasi kutoka nyuma.

Shirika la habari la Jiji lilisema serikali ya Japan imebuni jopokazi kuchunguza tukio hilo huku viongozi wakianza kulaani kitendo hicho.

“Tumehuzunishwa na kushangazwa na tukio la kupigwa risasi kwa waziri mkuu wa zamani Abe Shinzo,” Balozi wa Amerika nchini Japan Rahm Emanuel akasema kwenye taarifa.

“Serikali ya Amerika na raia wake wanaomba afueni ya haraka ya Abe na kutoa pole kwa familia yake na watu wa Japan,” akasema.

Mshauri maalum wa Waziri Mkuu Fumio Kishida, Gen Nakatani aliwaambia wanahabari kwamba “vitendo vya kigaidi sawa na hiki havitavumiliwa nchini.”

Abe ndiye waziri mkuu wa Japan ambaye amehudumu kwa miaka mingi zaidi.

Aliingia mamlakani kwa mwaka mmoja mnamo 2016 na kisha akahudumu tena kuanzia 2012 hadi 2020.Baadaye alilazimika kuondoka mamlakani kutokana na matatizo ya kiafya.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi, wakazi wamkosoa Ruto kuhusu kafyu Marsabit

Maadhimisho ya Idd yaanza leo Jumamosi wauzaji mifugo...

T L