• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Viongozi, wakazi wamkosoa Ruto kuhusu kafyu Marsabit

Viongozi, wakazi wamkosoa Ruto kuhusu kafyu Marsabit

NA JACOB WALTER

BAADHI ya viongozi na wakazi wa Marsabit, wamemkashifu Naibu Rais, Dkt William Ruto kutokana na matamshi yake kuwa kafyu iliyowekwa na serikali katika kaunti hiyo kukabiliana na utovu wa usalama itaondolewa akiwa rais.

Akiwa katika kampeni za kusaka uungwaji mkono mjini Marsabit, Naibu Rais mnamo Jumatano alisema kuwa kafyu hiyo iliyowekwa na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i Mei imesambaratisha uchumi wa eneo hilo.

Aliahidi kuwa akichaguliwa Rais kwenye uchaguzi wa Agosti 9, ataiondoa mara mojaHata hivyo, mwaniaji wa ubunge wa Saku kwa tikiti ya Wiper Barille Abduba alimkashifu Dkt Ruto na kusema kuwa kafyu hiyo imesaidia sana katika kudumisha usalama.

“Matamshi ya Dkt Ruto hayaakisi hali halisi nyanjani. Hakika kafyu hiyo imesaidia na hata tunataka maafisa zaidi wa usalama waongezwe hapa,” akasema Bw Abduba.

Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa kauli ya Dkt Ruto inaonyesha kuwa hafahamu kuwa wakazi wa Marsabit walikuwa wamechoshwa na mauaji ya mara kwa mara na kuharibiwa kwa mali yao.

Alikariri kuwa haingekuwa kuwekwa kwa kafyu hiyo, viongozi wa kisiasa akiwemo Dkt Ruto hawangekanyaga kaunti hiyo kuendeleza kampeni za kusaka kura.

Tangu kuwekwa kafyu hiyo vita vya kikabila na ukoo vimepungua sana na hakuna vifo vingi ambavyo vimeripotiwa ikilinganishwa na hapo awali. Utulivu umerejea huku wafanyabiashara nao wakiendelea na shughuli zao bila tatizo lolote.

Naye Diwani wa Marsabit ya Kati Isacko Kunni alisema wakazi hawana tatizo na kafyu na wanataka operesheni ya kuwaondoa majangili wanaodhaminiwa na wanasiasa uimarishwe hata zaidi.

Bw Kunni alilalamika kuwa bado kuna bunduki nyingi miongoni mwa wahalifu ambazo zinastahili kutwaliwa na maafisa wa usalama wanaoendeleza operesheni za kutwaa silaha haramu.

Pia mkazi Daudi Fille Dache alimkashifu Dkt Ruto akisema kuwa wakazi walifurahisha na matunda ya amani yaliyopatikana baada ya kuwekwa kwa kafyu hiyo.

“Kama mkazi wa hapa nimesikitishwa sana na matamshi ya Dkt Ruto. Haingekuwa kafyu hii iliyowekwa, hapa mauaji yangekuwa yakiendelea na tungekuwa tunaishi kwa hofu,” akasema Bw Dache.

  • Tags

You can share this post!

Sakaja kufahamu iwapo atawania ugavana Jumatatu

Aliyekuwa waziri mkuu wa Japan auawa kwa risasi

T L